Mwenyekiti wa Tume ya Madini asikitishwa na ukosefu wa uadilifu kwa Watumishi


Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Prof. Idris Kikula amekerwa na kukasirishwa na ukosefu wa uadilifu kwa wafanyakazi wa Tume ya Madini katika baadhi ya Ofisi na kueleza kuwa, suala hilo halitavumilika kwa wanaokwenda kinyume na maadili ya kazi.

Akizungumza na wafanyakazi wa Tume ya Madini Mkoa wa Morogoro katika siku ya kwanza ya ziara yake aliyoianza Aprili 8, 2019, Prof. Kikula amewaeleza wafanyakazi wa ofisi hiyo kuwa, yeye na viongozi wenzake wa tume wamekerwa na kusononeshwa na vitendo vya ukosefu wa uadilifu vinavyofanywa na baadhi ya wafanyakazi wa Tume ya Madini.

Ametolea mfano wa kitendo kilichofanywa na wanafanyakazi wa Tume hiyo wilayani Chunya ambapo watumishi wote wa kituo hicho wamesimamishwa kazi na Waziri wa Madini Doto Biteko kutokana na kukosa uadilifu na kutoa taarifa isiyo sahihi kwenye takwimu za madini.

“Kuna udanganyifu mkubwa unaofanywa na wachenjuaji madini, na udanganyifu huo unachochewa na watumishi wa Tume. Angalia mfano pale Chunya, wale wachenjuaji wamedanganya lakini ukifuatilia utagundua wafanyakazi wa tume wanahusika na huo udanganyifu, na ndio maana hata Waziri wa Madini aliamua kuchukua hatua ya kuwasimamisha kazi wafanyakazi wote wa kituo kile,” amesema Prof. Kikula.

Kufuatia hali hiyo, Prof. amekemea vitendo hivyo na kueleza kuwa, suala la uadilifu ni muhimu katika kazi za watumishi wa tume na kueleza kuwa, pamoja na kuwepo vishawishi vingi katika sekta ya madini, lakini wanapaswa kukumbuka kuwa kazi ni muhimu kwao na familia zao.

“Mimi na wenzangu tunaumizwa moyoni tunapoona wafanyakazi wa Tume wanakutwa na hatia ya ukosefu wa uadilifu inatusikitisha sana, sana”, amesisitiza Prof. Kikula.

Akitolea ufafanuzi kuhusu masuala mbalimbali yaliyowasilishwa na Kaimu Afisa Madini Mkazi, Prof. Kikula  amewapongeza watumishi  wote wa kituo cha madini Morogoro kwa kazi nzuri ya kusimamia ukusanyaji wa maduhuli na kuwaomba kuongeza bidii ili wafikie malengo waliyojiwekea.

Kuhusu masuala ya leseni, Prof. Kikula amemuagiza Kaimu Afisa Madini Mkazi kufuatilia leseni zote zilizopo na kubainisha leseni ambazo sio hai na kuzifuta kwa mujibu wa sheria. Aidha, amekumbusha kuhusu kufuata utaratibu halali uliowekwa kwa mujibu wa sheria katika hatua za ufutaji wa leseni hizo na kusema “asimuogope mtu lakini pia asimuonee mtu katika hatua hiyo ya ufutaji wa lesini zisizo hai”.

Aidha, Prof. Kikula amekiri kuwepo kwa changamoto na kuwataka watumishi hao kuwa na subira na kuongeza kuwa, Tume imepanga kununua magari 34 ambayo yatasambazwa katika mikoa yote ili kuongeza tija. Prof. Kikula amezungumza hayo baada ya kuwasilishwa kwa taarifa ya ofisi hiyo ambayo ilieleza kuwepo kwa changamoto kadhaa.