Nyaya za mawasiliano katika maduka ya vifaa vya kielektroniki yazuiliwa na TBS





Shirika  la Viwango Tanzania (TBS) limepiga marukufu kuuzwa kwa nyaya za kupitia mawasiliano (Data Cable) zilizokuwa zikiuzwa kwenye baadhi ya maduka ya vifaa vya kielektroniki baada ya kubainika hazikidhi viwango.

Hatua hiyo ilifikiwa na maofisa wa shirika hilo kwenye baadhi ya maduka jijini Dar es Salaam baada ya sampuli za nyaya hizo kupimwa kwenye maabara na kudhibitika hazikidhi viwango.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana Mkaguzi wa TBS, Saimon Emmanuel, amesema tayari wenye maduka yaliyokuwa yakiuza nyaya hizo wamepewa muda wa siku 14 kujieleza .

Pia amesema baada ya kupimwa kwenye maabara za shirika pamoja na kasoro nyingine, nyaya hizo zilibainika kuwa na kiwango kidogo cha madini ya shaba (copper) na kwamba hata nguvu kinzani kwenye nyaya hizo zilifeli kwenye maabara .

"Hivyo tumezizuia kwenye maduka tukisubiri hatua nyingine," amesema na kutoa mwito kwa wafanyabiashara wanapotaka kununua bidhaa kutoka nje ya nchi kuhakikisha zinakaguliwa ubora wake nje ya nchi kabla hazijaingia nchini mpangao ambao kitaalamu unaojulikana kama kama Pre-Shipment/Export Verification of Conformity to Standards (PVoC).

Pia ameongeza kuws wanaoingiza bidhaa kutoka nje ya nchi bila kukabuliwa kupitia PVoC, pindi bidhaa zao zinapofika nchini wanatozwa faini ya asilimia 15 kulingana na thamani ya mzigo, kulipia gharama za upimaji kwenye maabara na kwamba zinapofeli kufikia viwango muagizaji anaamuriwa kuzirudisha alikozitoa kwa gharama zake au kuteketezwa hapa nchini pia kwa gharama zake.

Emmanuel amesema hiyo ni kwa mujibu wa Sheria Na:2 ya Viwango ya mwaka 2009. Ametoa mwito kwa wafanyabiashara kuhakikisha wazingatia sheria na taratibu ili kuepuka hasara.

Shirika hilo kwa sasa linaendesha awamu ya pili ya msako wa kushtukiza wa bidhaa zilizopo sokoni ili kubaini bidhaa ambazo hazina ubora na kuziondoa kwenye soko.