Ofisi ya Utumishi yaanza kutoa huduma kwenye Mji wa Serikali


Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeanza kutoa huduma katika ofisi zake kwenye Mji wa Serikali, Mtumba jijini Dodoma baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kuzindua ofisi za Wizara zilizojengwa katika mji huo kwa ajili ya kutoa huduma kwa wananchi.

Akizungumzia kuhusu utoaji wa huduma katika Mji wa Serikali, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amesema, ofisi yake iko tayari na imejipanga kikamilifu kutoa huduma kwa wananchi na wadau wote wa masuala ya kiutumishi na utawala bora.

Dkt. Ndumbaro ametoa wito kwa wananchi, watumishi wa umma na wadau wengine kufuata huduma katika ofisi yake iliyopo Mtumba kwenye Mji wa Serikali na kuongeza kuwa, kwa sasa Idara zilizohamia ni ya Utawala na Utumishi wa Umma na ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu ambazo zina wateja wengi, hivyo watumishi wa umma na wananchi wajitokeze kupata huduma.

Aidha, Dkt. Ndumbaro amesisitiza kuwa, mwananchi au mtumishi yeyote mwenye uhitaji wa kupata huduma kutoka kwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu wafike katika ofisi za Mtumba ili waweze kuhudumiwa ipasavyo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli tarehe 13 Aprili, 2019, alizindua rasmi ofisi za wizara zilizojengwa katika Mji wa Serikali na kuelekeza Watumishi waanze kutoa huduma kwa wananchi mapema iwezekanavyo.