RC asikitishwa na maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya


Na. Enock Magali, Dodoma

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dk. Binilith Mahenge ameonyesha kusikitishwa na maendeleo ya ujenzi wa Hospital ya Wilaya ya Chemba na hivyo kuagiza hadi kufikia mwezi May mwaka huu ujenzi huo kuwa umekwisha kamilika.

Dk. Mahenge ametoa maagizo hayo Leo mara baada ya kufanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Hospital hiyo ambapo amewataka Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha wanaondoa vikwazo vyote vinavyopelekea ucheleweshaji wa ujenzi huo ikiwa ni pamoja na kuongeza mafundi ili kazi iende kwa uharaka zaidi.

"Mara ya kwanza nilipokuja hapa niliwapongeza, niliona mna hatua nzuri ya msingi lakini leo hapana inaelekea mna vitu vingi vinavyowachelewesha kwaiyo nawaomba muondoe vile vikwazo vyote vidogo vidogo vinavyo wakwamisha, lakini la pili hakikisheni mnaongeza mafundi msimuachie mtu mmoja" alisema Mahenge

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo Saimon Odunga amesema atakaa na kuzungumza na mafundi hao ili kujua changmoto inayowakwamisha ambapo hata hivyo watalazimika kuongeza mafundi ili kuhakikisha kazi hiyo inakwenda kwa haraka zaidi.

"Tutakaa tena na hawa mafundi kuona wamekwama wapi,nilipokuwa nikizungumza nao jana waliniambiwa mafundi waliopo wanatosha, na huu ukuta unaouona umejengwa kwa siku mbili yaani jana na leo na wakanihakikishia kuwa baada ya siku mbili nyingine watakuwa wamefikia hatua ya kufunga lenter lakini kwa maagizo yako Mkuu wa Mkoa tutakaa nao ili waongeze mafundi wengine,” alisema Odunga

Wakizungumzia madai ya mafundi kutolipwa fedha zao Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo Dr.Semistatus Mashimba na kaimu mhandisi wa wilaya hiyo Filomena Bango wao wamekanusha madai hayo na kusema kuwa mafundi wote wakwishalipwa fedha zao katika awamu ya kwanza ya ujenzi ambayo imekwishakamilika.

Hata hiyo mara baada ya baadhi ya mafundi kuhojiwa juu ya madai ya kutolipwa fedha zao mafundi hao wamekana na kusema kuwa wamekuwa wakilipwa fedha zao kwa wakati na hadi sasa wanaendelea na kazi vizuri.