.

4/15/2019

RC Makonda atoa agizo zito kwa DC Kinondoni na Mkurugenzi


Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda leo ameendelea na ziara ya kikazi ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo Wilaya ya Kinondoni na kumtaka Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi kutowachekea watu wanaoonekana kuwa na ubabaishaji kwenye utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Akiwa katika Miradi wa Barabara ya Kituo cha Mabasi cha Simu2000 RC Makonda ameshangazwa na Gharama kubwa inyotumika kujenga barabara za DMDP tofauti na Zile za TANROAD na TARURA ambazo zinajengwa kwa kiwango sawa lakini kiasi cha pesa ni kidogo huku Wakandarasi wa DMDP wakijiamulia kupandisha gharama za Ujenzi kutoka Billion 8 hadi Billion 13 jambo ambalo ametaka kuangaliwa kwa jicho la tatu.

Aidha RC Makonda ameitaka Manispaa ya Kinondoni kutoruhusu Mshauri wa Mradi wa Soko la kisasa Magomeni kubadili vipimo vya Urefu wa jengo na ukubwa wa Vizimba tofauti na Mchoro uliopendekezwa jambo litakalokuja kuleta usumbufu mkubwa kwa miaka ijayo.

Akiwa katika ukaguzi wa miradi ya Ujenzi wa Hospital ya Kigogo, Kituo cha Afya Msasani, Barabara ya Kigogo Barafu, Soko la Magomeni, Soko la Afrikasana, Barabara ya Mabatini, Barabara ya Makanya, Barabara ya Tandale na Shule ya Sekondari Mzimuni RC Makonda ameitaka manispaa ya Kinondoni kuimarisha usimamizi wa miradi hiyo na kuhakikisha inakamilika kwa wakati.

Pamoja na hayo RC Makonda amewataka wasimamizi wa miradi ya Ujenzi kuacha unyonyaji wa kuwalipa vibarua kiasi cha Shilingi 7,000 au 8,00e0 kwa siku badala ya 12,500 inayotambulika kiserikali.