RC Makonda azidi kufichua madudu miradi DMDP


Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda amemuagiza Mkurugenzi wa TAKUKURU Mkoa huo kufanya uchunguzi wa utaratibu wa upatikanaji wa tenda kwenye miradi ya DMDP baada ya kubaini matumizi mabaya ya fedha za serikali katika miradi hiyo.

RC Makonda amesema haiwezekani kuona Kilomita Moja ya Barabara ya DMDP Wilaya ya Kinondoni inajengwa kwa Shilingi Billion 2.7 wakati kwa Wilaya ya Temeke barabara kama hiyo inajengwa kwa shilingi Milioni 900.   

Mhe. Makonda amebaini madudu hayo wakati wa mwendelezo wa ziara yake ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo kupitia fedha zinazotoka Serikali Kuu, Halmashau na pesa za wahisani ambapo amekwazwa na matumizi mabaya ya fedha za mkopo kutoka Bank ya dunia.

Aidha RC Makonda amesema kuwa Barabara  za DMDP zimekuwa zikijengwa kwa kiasi kikubwa cha pesa kuliko zile za TANROAD ambazo kwanza zina ubora mkubwa, uwezo wa kubeba mzigo mkubwa na pia ni Pana.

Katika ziara hiyo RC Makonda ametembelea miradi ya Ujenzi wa Barabara,Hospital na Shule ambapo ameipongeza Manispaa ya Temeke kwa kusimamia vizuri miradi ya Maendeleo na kuwataka kuongeza kasi.