RC Mnyeti azindua kampeni ya Jiongeze tuwavushe salama


Na John Walter-Manyara

Mkuu wa mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti amesema ili kuweza kuhakikisha mama mjamzito na mtoto wanakuwa salama ni lazima familia,jamii,taasisi za dini,wadau wa maendeo na serikali ziweke na kuongeza juhudi katika kudhibiti vifo hivyo.

Amesema ili kufanikisha hilo lazima kuwepo mikakati madhubuti katika kusimamia utekelezaji wake ili kuweza kuhakikisha hilo linafanikiwa.

Mnyeti ameyasema hayo wakati akizungumza na wakuu wa wilaya,wakurugenzi,madaktari,wauguzi na wadau mbalimbali wa fya mkoani hapa kwenye uzinduzi wa kampeni ya “Jiongeze Tuwavushe Salama”  ambayo Kitaifa ilizinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan Oktoba 7,2018 jijini Dodoma.

Amesema katika mkoa wa Manyara hataki kusikia Mama mjamzito anatozwa pesa  anapokwenda kupata huduma au kujifungua kwa kuwa serikali imeshatoa maagizo kuwa huduma hizo ni bure huku akimtaka mganga mkuu  kuanza kuwawajibisha wanaofanya hivyo pomoja na kuwachukulia hatua  madaktari na wauguzi wanaozembea kufanya kazi hali inayopelekea wagonjwa wengi haswa wakinamama wajawazito na watoto kupoteza maisha pindi wanapofika hospitalini kujifungua.

Kampeni hiyo maalum inaongozwa na ujumbe  usemao “Jiongeze tuwavushe Salama,Kila mmoja wetu ana wajibu wa kuzuia vifo vitokanavyo na uzazi na vya watoto.Maneno sasa basi,Sasa Vitendo”.

 Aidha ameingia mikataba ya makubaliano na  wakuu wa wilaya juu ya kutekeleza maazimio yote katika maeneo yao na kuhakikisha kampeni hiyo inatekelezwa ipasavyo katika ngazi zote kwenye maeneo yao.

Katika hatua nyingine Mnyeti amesema,mkoa wa Manyara umepokea shilingi Bilioni 6.9 kutoka serikali kuu kwa ajili ya ujenzi wa hospitali mpya katika wilaya ya Mbulu na ukarabati wa vituo tisa vya afya Vya Sunya wilaya ya Kiteto,Dongobesh,Daudi na Tlawi katika wilaya ya Mbulu,Magugu na Nkaiti za wilaya ya Babati,Simbay na Hilbadaw za Hanang pamoja na Orkesumet wilaya ya Simanjiro.