Serikali kuleta mabehewa na vichwa vya treni ya umeme 1,400


Serikali imesema inakamilisha taratibu za kuleta mabehewa na vichwa takribani 1,400 vya treni ya umeme.

Hayo yamebainishwa na Msemaji wa Serikali, Dkt. Hassan Abbas kupitia ukurasa wake wa Mtandao wa Kijamii wa Twitter alipokuwa akizungumzia tukio la uungwaji wa reli ya treni za Umeme, Standard Gauge Railway(SGR)

Kuunganishwa kwa vipande vya SGR ili kufanya reli hiyo kuwa moja kutoka Morogoro hadi Dar ikiwa ni awamu ya kwanza ya ujenzi kulifanyika jana Aprili 14, 2019 katika kijiji cha Soga mkoani Pwani na kuhudhuriwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe

Waziri Kamwelwe alieleza kuwa ifikapo mwezi wa saba mwaka huu, Mkandarasi wa reli hiyo na Shirika la Reli nchini(TRC) wataleta kichwa cha treni ya umeme kwa ajili ya majaribio kwenye kipande cha reli cha Kilometa 30