Serikali Mbioni kuanza mpango wa uagizaji wa Gesi ya mitungi kwa pamoja


Serikali iko katika hatua za awali za kuandaa mpango wa uagizaji wa gesi ya mitungi (LPG) kwa pamoja kama ilivyo kwa mafuta ya Petroli hali itakayosaidia kudhibiti masuala mbalimbali ikiwemo  bei ya gesi hiyo .


Akizungumza wakati wa semina kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini iliyofanyika jijini Dodoma, Waziri wa Nishati, Dkt Medard Kalemani alisema kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa, wananchi katika maeneo yote nchini wanafikiwa na huduma hiyo, hivyo Serikali itaratibu usambazaji wa gesi hiyo badala ya kuwaachia wauzaji wenyewe kuamua maeneo  wanayotaka kupeleka gesi.

“Serikali ikitangaza bei elekezi kulingana na soko, itawafanya wauzaji wafuate bei hiyo badala ya wao kujipangia, hii itasaidia wananchi kuuziwa gesi kwa gharama inayofanana katika maeneo mbalimbali ambapo gesi hiyo itauzwa.”alisema Dkt. Kalemani.

Alieleza kuwa, suala la sasa la kila muuzaji kujiamulia sehemu anayotaka kupeleka gesi inafanya maeneo mengine kukosa kabisa nishati hiyo hivyo sasa Serikali itaweza kuwadhibiti wauzaji na kuhakikisha kuwa maeneo yote nchini yanafikishiwa gesi.

Aliongeza kuwa, utaratibu wa kuagiza gesi inayotumika  majumbani kwa pamoja utasaidia Taifa kutambua kiwango halisi cha gesi kinachohitajika nchini na kiasi cha gesi kinachoingizwa nchini na hivyo kusaidia pia katika shughuli za ukusanyaji wa mapato.

Awali, akitoa taarifa kwa Wajumbe wa Kamati hiyo, Kaimu Mkurugenzi  Mkuu wa Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja  (PBPA), Erasto Simon  alisema kuwa, Wakala huo kwa sasa unafanya tathmini ya namna bora ya kuanza uagizaji wa pamoja wa gesi ya mitungi (LPG) kwa kuzingatia maoni kutoka kwa  wadau mbalimbali.


Akizungumzia faida mbalimbali zinazotokana na uagizaji wa mafuta wa pamoja, Simon alisema kuwa, ni kuweka mazingira sawa ya kibiashara kwani gharama za uagizaji wa mafuta ziko sawa kwa makampuni yote na kuondoa mianya ya rushwa katika uagizaji wa mafuta kwani ufunguzi wa zabuni hufanyika kwa uwazi na washiriki wote huridhika na matokeo ya zabuni.