Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Norway nchini Bi. Elisabeth Jacobsen katika ofisi za Wizara zilizopo jijini Dodoma.
Katika mazungumzo hayo yaliyolenga uboreshaji wa sekta ya afya nchini, Balozi Elisabeth amesema Serikali ya Norway itaendelea kusaidiana na Serikali ya Tanzania katika kuboresha sekta ya afya hasa katika kukabiliana na magonjwa ya Malaria, Kifua Kikuu, UKIMWI na ukosefu wa lishe bora.
Bi. Elisabeth amesema Serikali ya Norway itaendelea kuisaidia Tanzania katika sekta ya afya kupitia Shirika la GAVI ambalo linajihusisha na ununuaji na usambazaji wa chanjo kwa nchi wanachama wa shirika hilo.
Aidha, Balozi huyo amesema kupitia mfuko wa Global Fund utawezesha Serikali kukabiliana na magonjwa ya Malaria, TB na UKIMWI na hivyo kuwezesha Tanzania kuwa miongoni mwa nchi zitakazofikia malengo ya maendeleo endelevu yaliyoanzishwa na Umoja Mataifa.
Kwa upande wake Waziri Ummy amemuomba Balozi huyo kupitia Serikali ya Norway kuisadia Serikali katika vita dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa kuwezesha kutoa elimu ya usawa wa kijinsia ikiwa ni pamoja na kumuelimisha mtoto wa kike.
Pia Waziri Ummy amemuomba Balozi huyo kuisadia Serikali katika kutoa mikopo kwenye vikundi vya wanawake ili waweze kujihushisha na shughuli za maendeleo na kujikwamua kiuchumi na kuisaidia familia.
Kwa upande wa lishe, Waziri Ummy amesema Serikali imeshaanza uhamasishaji wa Lishe Bora kupitia taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) kwa kutoa elimu ya lishe kwa watoto walio chini ya miaka mitano ili kukabiliana na udumavu ambao kwa kiasi kikubwa umeathiri ukuaji wa watoto katika baadhi ya mikoa nchini.