Shambulizi la anga lamuua Naibu mkuu wa ISIS eneo la Putland Somalia



Kamanda wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) ameripotiwa kuuawa katika shambulizi la anga lililofanyika katika eneo lenye mamlaka ya ndani la Puntland nchini Somalia.

Waziri wa Usalama wa Puntland, Abdisamad Mohamed Galan ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa, Abdihakim Dhuqub, Naibu Kamanda wa ISIS aliuawa katika hujuma ya anga ya jana Jumapili, katika kijiji cha Xiriiro, kilichoko katika eneo la milima la Qandala.

Amesema kiongozi huyo wa ngazi za juu wa ISIS ambaye kitambo alikuwa mwanachama wa al-Shabaab ameuawa pamoja na makamanda wengine kadhaa wa genge hilo la ukufurishaji katika shambulizi hilo la jana lililofanywa katika eneo leye milima mingi la Bari.

Mohamed Iid, mkazi wa kijiji cha Xiriiro amesema gari aina ya Suzuki 4x4 lilokuwa limembeba kamanda huyo wa ISIS lililengwa kwa makombora matatu katika hujuma hiyo ya jana, yapata kilomita 3 nje ya kijiji hicho kilichoko katika eneo la Puntland.


Matt Bryden, mkuu wa kituo cha wanafikra na utafiti cha Sahan chenye makao makuu yake katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi amesema genge la ISIS lenye wanachama kati ya 150-200 nchini Somalia halina nguvu na halijakuwa likifanya mashambulizi ya kutisha ikilinganishwa na jinai za al-Shabaab.
Hata hivyo anasisitiza kuwa kundi hilo linapaswa kutokomezwa kabla halijawa genge kubwa na kupanua mbawa zake.