Tundu Lissu aeleza maendeleo ya afya yake


Mwanasiasa wa upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki amesema hali yake ya kiafya inaendelea vizuri.

Mwanasheria huyo Mkuu wa CHADEMA amesema Sasa kazi kubwa iliyobaki ni kukunja goti na kujifunza kutembea tena.

"Mfupa wote wa mguu wa kulia umepona vizuri. Sehemu iliyowekewa 'kiraka' cha mfupa na kupigwa 'ribiti' ya chuma juu kidogo ya goti; na sehemu ya kwenye paja iliyotakiwa kuota mfupa mpya, zote ziko vizuri," amesema Lissu.

Ameendelea kwa kusema kuwa, 'Tarehe 14 ya mwezi ujao nitapimwa urefu wa miguu ili nitengenezewe kiatu au soli maalum kwa ajili ya mguu wa kulia.Kwa sababu ya majeraha makubwa niliyopata, mguu huo ni mfupi kwa sentimita kadhaa. Bila kiatu au soli maalum nitakuwa 'langara' sana na madaktari wamesema hiyo sio sawa sawa'.

Utakumbuka Septemba 7, 2017 Tundu Lissu alishambuliwa na kujeruhiwa vibaya kwa risasi
akitokea Bungeni Jijini Dodoma. Lissu alipatiwa matibabu ya mwanzo nchini Kenya kisha kuhamishiwa Ubelgiji.