https://monetag.com/?ref_id=TTIb Ufaransa yakanusha tuhuma za Libya | Muungwana BLOG

Ufaransa yakanusha tuhuma za Libya


Ufaransa imekanusha tuhuma kutoka wizara ya mambo ya ndani ya Libya kwamba imekuwa ikimuunga mkono mbabe wa kivita, Jenerali Khalifa Haftar, ambaye jeshi lake limeanzisha operesheni ya kuutwaa mji mkuu wa nchi hiyo, Tripoli.

Taarifa ya wizara hiyo iliyotolewa jana inasema imesitisha mahusiano yote kati yake na upande wa Ufaransa kutokana na msimamo wa serikali ya Ufaransa kumuunga mkono inayemuita kuwa ni mhalifu Haftar.

Wizara ya mambo ya nje ya Ufaransa imeziita tuhuma hizo kuwa za kuudhi na za uzushi. Taarifa ya ikulu ya Ufaransa imesema kuwa nchi hiyo inaiunga mkono serikali ya Libya inayotambuliwa kimataifa chini ya Waziri Mkuu Fayez al-Sarraj na pia "juhudi za upatanishi za Umoja wa Mataifa kuelekea suluhisho la kisiasa linalojumuisha pande zote."

 Ufaransa imesaidia kutoa mafunzo kwa vikosi vya usalama vya Libya vilivyo chini ya serikali mjini Tripoli, wakiwemo polisi na walinzi wa Waziri Mkuu Sarraj.