UN yawahamisha wakimbizi kutoka Libya


Umoja wa Mataifa umesema umewahamishia Niger wakimbizi 163 kutoka Libya, huku zaidi ya 3,000 wengine wakiwa bado wamekwama kwenye vituo vya kuhifadhi wahamiaji ambavo pia vimeathiriwa na mapigano.

Kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR hii ni mara ya kwanza wanawahamisha wakimbizi hao kutoka Libya tangu kuzuka kwa mapigano katika mji wa Tripoli wiki mbili zilizopita.

 Mkuu wa shirika hilo la UNHCR Filippo Grandi amesema hatua hiyo inafuatia hali ilivyo nchini Libya. Operesheni hiyo inakuja kufuatia mapigano makali yanayoendelea kati ya vikosi tiifu kwa generali muasi Khalifa Haftar na yale yanaonga mkono serikali inayotambulika na jumuiya ya kimataifa.

Wanawake na watoto ni miongoni mwa waliohamishwa mapema hii leo. Shirika la afya la Umoja wa Mataifa limesema mapigano hayo mapya yamesababisha vifo vya watu 200 na wengine 900 kujeruhiwa.