Urusi kuunda Intaneti yake binafsi


Bunge la taifa la Urusi maarufu Duma limepitisha mswada ambao utakapokuwa sheria basi taifa hilo litabuni mfumo wake pekee wa mtandao wa Intaneti ambao utalifanya taifa hilo kutotegemea Intaneti inayotumika duniani.

Mswada huo ambao ulipitishwa kwa kura nyingi za wabunge 307 huku 68 wakipiga kura kuupinga, utawasilishwa katika bunge kuu la Urusi ili kuidhinishwa na kisha kuwasilishwa kwa rais Vladmir Putin kutia sahihi ili kuwa sheria kamili na kuanza kutekelezwa Novemba, mosi mwaka huu.

Sheria hiyo itawezesha serikali ya Urusi kubuni miundo mbinu yao binfasi ya Intanet na kuweza kusalia mtandaoni lau kutatokea dharura ya taifa lolote kujaribu kuizima huduma za Intaneti.

Mmoja wa waandishi wa mswada huo Andrei Klishas aliye pia mwanachama wa bunge kuu aliliambia shirika la habari la DW kwamba hawana shaka Marekani ina uwezo wa kiufundi wa kuizimia Urusi huduma za Intaneti wakati wowote wakipenda kwa hivyo na wao wanajiandaa kiufundi kuhakikisha wanajilinda dhidi ya mashambulizi hayo.

Mkuu wa kamati ya sera na habari Leonid Levin alisema huduma salama za intaneti ni muhimu kwa warusi na serikali kwa jumla.

"Lengo la mswada huu ni kuhakikisha Intaneti inapatikana kwa Warusi iwe ni kutoka nje ya nchi ama ndani ya nchi. Kwa njia hii, huduma ya taifa za kieletroniki, huduma za benki kutumia mfumo wa Intaneti pamoja na huduma mbali mbali za biashara ambazo wananchi wamezizoea zitafanya kazi kwa usawa kabisa bila ya kufeli. mswada huu ni kuongeza upatikanaji wa intaneti ambayo inataegemewa Urusi kwa hivyo wanalifanya hilo kuhakikisha ustawi na ubora wake," alisema Leonid.