Wabunge wanaotumia simu kujirekodi sauti bungeni waonywa


Dk Tulia Ackson ambaye ni Naibu Spika wa Bunge la Tanzania,  amewaonya wabunge wanaotumia simu zao za mkononi kujirekodi sauti wakati muda wao wa kuchangia bungeni unakuwa umeisha.

Kauli hiyo imetolewa leo bungeni jijini Dodoma katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo  mwaka 2019/2020 baada ya mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), Joseph Mbilinyi  ‘Sugu’ kuendelea kuzungumza licha ya muda wake kumalizika.

“Waheshimiwa wabunge kabla hajasimama Mwamoto (Venance-Mbunge wa Kilolo-CCM) kuchangia naomba niwakumbushe tu.  Umezuka utaratibu hapa, nimezima kisemeo lakini Mbilinyi anaendelea kuzungumza,” amesema Dk Tulia.

“Halafu anakuwa yeye mwenyewe, jirani yake au rafiki yake anachukua maneno hayo kama mchango wake bungeni wakati yeye ameshakatwa. Mzifahamu vizuri kanuni zetu hairuhusiwi kwa sababu si mchango uliotoka bungeni.”

 Ameongeza, “Nyinyi mnaendelea kuzungumza wakati umekatazwa na mnatoa habari hiyo nje wakati si mchango uliochukuliwa. Tafadhalini sana tufuate utaratibu tuliojiwekea  wenyewe.

Aidha Dk. Tulia amesema wWbunge hao huchukua sauti hizo ambazo hazijaingizwa katika kumbukumbu za Bunge na kuzitumia maeneo mbalimbali na kuonekana ni kauli walizozitoa bungeni.