Wagonjwa wenye Saratani ya koo waanza kuwekewa vifaa tiba


Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imepata msaada wa vifaa tiba aina ya stents  kutoka Kampuni ya Boston Scientific ya Marekani vyenye thamani ya shilingi milioni 29 ambavyo vitawasaidia wagonjwa wenye tatizo la saratani ya koo la chakula.

Stents ni vifaa maalum mithili ya springi ambavyo vinaweza kuwa vya plastiki au chuma vyenye uwazi katikati wanavyowekewa wagonjwa wenye uvimbe kwenye koo lililoziba ili kupanua sehemu hiyo na kuruhusu kupitisha chakula. Kuna stents za aina mbalimbali kutegemeana na mgonjwa ana shida ya aina gani.

Msaada huo umetolewa leo kwa Muhimbili ikiwa ni matunda ya ushirikiano kati ya Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba (MUHAS), Taasisi ya Saratani Ocean Road na Chuo Kikuu cha San Francisco nchini Marekani.

Mratibu wa Utafiti wa magonjwa ya saratani kutoka taasisi ya MUHAS, OCEAN ROAD na UCSF, Dkt. Musiba Selekwa amesema Muhimbili imepatiwa stents 70 na kwamba wagonjwa wenye uhitaji watawekewa vifaa tiba hivyo ambavyo vitawasaidia kumeza chakula na kuendelea na matibabu mengine.

Amesema lengo la ushirikiano wa taasisi hizo ni kuwajengea uwezo wataalam wa afya wabobezi nchini pamoja na kuboresha huduma za matibabu kwa wagonjwa wa saratani ya koo nchini.

“Wagonjwa wenye uhitaji na ambao hawana uwezo wa kununua vifaa tiba watapunguziwa gharama ya vifaa tiba ili kuwawezesha watu wengi zaidi kupatiwa matibabu haya,” amesema Dkt. Selekwa.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Muhimbili, Prof. Lawrence Museru amesema wataalam kutoka Marekani wanaendelea kuwajengea uwezo wenzao wa Muhimbili na kutoa matibabu kwa wagonjwa mbalimbali wenye tatizo la saratani ya koo.

Mgonjwa mwenye tatizo la saratani ya koo la chakula, anakuwa hawezi kumeza chakula hivyo hali hiyo inasababisha mgonjwa kupungua uzito na kushindwa kuendelea na matibabu mengine, hivyo vifaa hivi vitawasaidia kumeza chakula na kuendelea na matibabu mengine.