Watu wapatao 32 wameuwawa kwenye mapigano Libya


Marekani imemtaka kiongozi wa kijeshi wa Libya, Khalifa Haftar asitishe haraka opereshini zake za kijeshi.

Mapigano kusini mwa mji mkuu Tripoli yanaendelea licha ya wito wa Umoja wa Mataifa wa kuweka chini silaha.

 Vikosi vya Haftar na vile vya serikali inayoungwa mkono na jumuia ya kimataifa vimeanza mashambulio ya angani jana, siku tatu baada ya Haftar na vikosi vyake kuanza opereshini ya kuukomboa mji mkuu Tripoli.

 Watu wasiopungua 32 wanasemekana wameuwawa hadi sasa. Umoja wa Mataifa ulitoa wito wa kusitishwa mapigano kwa masaa mawili ili kuwawezesha raia na majeruhi kuhamishwa.

Hujuma za vikosi vya Haftar zinatishia kuitumbukiza upya nchi hiyo katika janga la vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Zinatishia pia kukorofisha juhudi za upatanishi za Umoja wa mataifa. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, Mike Pompeo amesisitiza hakuna ufumbuzi wa kijeshi kwa mzozo wa Libya. Amezitolea wito pande zote zinazaohusika zirejee katika meza ya majadiliano.