Wauzaji wa Pembejeo Feki kwanini hawanyang'anywi leseni? - Bashungwa


Naibu Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa amewaelekeza Wadau wote kwenye mnyororo wa pembejeo kuwa sasa ni wakati wa kusimamia ipasavyo Sheria zote zinazohusu tasnia ya pembejeo kuanzia viutatilifu, mbegu pamoja na mbolea ili kumsaidia Mkulima mnyonge wa Tanzania.

Bashungwa ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa Wadau wa Pembejeo za kilimo ambapo Taasisi ya Udhibiti wa Mbegu Bora (TOSCI) imeandaa mkutano kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea (TFRA) na Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu katika Ukanda wa Kitropiki (TPRI) kwa lengo la kufanya tathmini ya maboresho ya mambo kadhaa yenye lengo la kuboresha utendaji kazi wa Taasisi hizo kwa pamoja.

Naibu Waziri Bashungwa amesema Mkulima wa Tanzania amekuwa akikabiliwa na changamoto nyingi wakati wa kuendesha kilimo chake na kuongeza kuwa changamoto hizo ni pamoja na viuatilifu ‘feki’, mbegu hafifu na ‘feki’ pamoja na mbolea ‘feki’ sasa zinapaswa kuisha kwa kuwa Taasisi zote zimepewa mamlaka ya kumkamata na kumfungulia mashitaka muuzaji yeyote atakaye kutwa akiuza au kusambaza pembejeo ‘feki’ na kuongeza kuwa amekuwa akishangazwa na kasi ndogo ya utekelezaji wa jambo hilo.

“Ndugu zangu Wataalam nimekuwa nikisikia na kuona idadi ndogo ya Wasambazaji na Wauzaji wa pembejeo feki wanaokamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria, tofauti na idadi kubwa ya malalamiko ya Wakulima wetu, sasa iwe mwisho, Wasambazaji na Wauzaji wanafahamika, simamieni sheria, wakamatwe na wafikisheni kwenye vyombo vya sheria na wanapopatikana na hatia, wafungwe kwa mujibu wa sheria.” Amekaririwa Waziri Bashungwa.

“Si sawa Wasambazaji feki wa pembejeo kuendelea na mchezo huu, huu ni wakati wa kuwadhibiti na kuwafunga, kwa sababu sheria zipo na zinasema wazi wazi, adhabu ya Mtu anayefanya kosa hilo” Amekaririwa Mhe. Bashungwa.

Naibu Waziri Bashungwa ameagiza kuwa mbali na mambo mbalimbali watakayojadiliana katika mkutano huo msisitizo lazima uwekwe kwenye kutafu njia bora ya kuongeza ufanisi na kuondoa changamoto kwenye upatikanaji na utoaji wa huduma ya usambazaji wa pembejeo bora kwa Wakulima na kama kuna vikwazo vyovyote mkutano huo utoe mapendekezo kwa Wizara nini kifanyike.