Loading...

5/17/2019

Bunge laagiza madeni ya Wizara ya Ulinzi yalipwe


Bunge limeitaka serikali kuongeza kasi ya ulipaji wa madeni ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa kuongeza fedha kwenye fungu la miradi ya maendeleo ya wizara hiyo.

Akiwasilisha bungeni jijini Dodoma , maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama, mjumbe wa kamati hiyo, Victor Mwambalaswa, alisema katika mwaka huu wa fedha, kati ya Sh. bilioni 112.6 zilizotengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, Sh. bilioni 105.2 (asilimia 93) zilitumika kulipa madeni ya mikataba.

Mwambalaswa alisema kulipa madeni hayo kwa wakati kutasaidia serikali kuokoa fedha zinazoongezeka kwaajili ya malipo ya riba na kuelekeza fedha kwenye maeneo mengine.

"Serikali itoe fedha zote za maendeleo zilizoidhinishwa kwa ajili ya Fungu la 38 kwa mwaka wa fedha 2018/2019. Hadi kufikia Machi 2019, fungu hili lilikuwa limepokea Sh. bilioni 3.34 kati ya Sh. bilioni nane zilizokuwa zimeidhishwa na Bunge, sawa na asilimia 41.83.

"Sambamba na ushauri huo, serikali ione umuhimu wa kuongeza fedha za maendeleo zilizotengwa kwa mwaka 2019/2020 na kutoa fedha hizo kwa wakati," alisema.

Loading...