Hakuna maana kuwa na mashirika yanayofanya kazi kwa hasara - Rais Magufuli


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo amepokea Gawio la Tsh.  Bilioni 2.1 kutoka Shirika la Mawasiliano ya Simu Tanzania (TTCL), ikiwa ni faida iliyotokana na maboresho makubwa yaliyofanywa na shirika hilo, hivyo kujiendesha kwa faida tofauti na awali wakati lilipokuwa limebinafsishwa .

Rais Magufuli ameelezea kufurahishwa kwake na mafanikio makubwa ya shirika hilo kutokana na historia kwamba shirika hilo kwa kipindi cha miaka 15 iliyopita, lilikuwa likijiendesha kihasara bila kutoa hata gawio kwa serikali wakati lilipokuwa limebinafsishwa.

"Baada tu ya Serikali kuichukua TTCL, Shirika hili limeanza kufanya vizuri, kwa mwaka huu limepata faida ya shilingi Bilioni 8.3 na wameweza kutoa gawio Serikalini kwa miaka miwili mfululizo," amesema Rais Magufuli.

Katika hatua nyingine amesema kuwa, "Msajili wa Hazina hakikisha ifikapo mwezi Julai, Mashirika yote 253 nchini ambayo yamekuwa hayatoi gawio kwa Serikali, yawe yametoa gawio, la sivyo yafungwe. Kama Shirika halitoi gawio kwa sababu linajiendesha kwa hasara basi lifungwe, hakuna maana kuwa na Mashirika yanayofanya kazi kwa hasara, la sivyo watafute namna ya kutoa magawio yao Serikalini,".

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TTCL Corporation, Mhandisi Waziri Kindamba amesema wamejipanga katika maeneo makuu matatu ikiwemo kuboresha huduma, uwezo wa kiteknolojia, ambayo Rais Magufuli ameshuhudia leo wakati akizungumza na baadhi ya wakuu wa mikoa kutoka Tanzania, wakiwa katika maeneo yao ya kazi pamoja na usimamizi mahiri wa mkongo wa Taifa ambao umepanuka na kutoa huduma katika nchi za jirani kiwemo Uganda, Rwanda, DRC Congo, na Zambia.