Kiwanda cha kuchakata Korosho kujengwa Mtwara


Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amesema serikali inajenga kiwanda cha kuchakata mazao ya korosho ili kuzalisha, kutengeneza juisi na mvinyo Naliendele Mtwara.

Waziri Hasunga alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Ndanda, Cecily Mwambe (Chadema), aliyetaka kujua utafiti wa kuongeza thamani mazao ya korosho (mabibo) umefikia wapi na lini juisi na mvinyo zitaanza kutengenezwa katika Kituo cha Utafiti Kilimo cha Naliendele (NARI) Mtwara.

Hasunga alisema ni kweli utafiti wa kina ulifanyika kuhusu namna ya kuongeza thamani mazao ya korosho (mabibo) ili kutengeneza juisi na mvinyo na maagizo yaliyopo ni kujenga kinu cha kuchakata mazao hayo ili kutengeneza vinywaji hivyo.

Akijibu swali la msingi la Mbunge wa Muheza, Balozi Adadi Rajab (CCM) aliyetaka kujua kwa nini serikali isiondoe sera ya viwanda kuhusu zao la chai ambayo hairuhusu wakulima wa chai kufungua viwanda wenyewe ili kuiongeza thamani chai hivyo kufanya Kampuni ya East Usambara Tea Co. Ltd (EUTCO) iliyopo Amani isiathirike. Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Stella Manyanya alisema utaratibu wa kuanzisha viwanda vya chai unafanyika kwa kufuata sheria ya chai namba 2 ya mwaka 1997 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2009 na kanuni zake za 2010.

Alisema sheria hiyo inamtaka mwombaji wa leseni ya kuanzisha kiwanda cha kusindika majani mabichi au kuchanganya chai kukidhi vigezo vinavyotakiwa. "Mnyororo wa uzalishaji wa zao la chai unahusisha hatua mbili ambazo ni usindikaji wa majani mabichi ili kuzalisha chai kavu na uchanganyaji na uwekaji wa chai kwenye vikasha kwa ajili ya kuuzwa sokoni,"alisema.

Alisema kampuni ya EUTCO ni miongoni mwa wakulima wakubwa wa chai hapa nchini wenye viwanda vitatu vya kusindika majani mabichi ya chai ikiwa ni hatua za awali ya kuongeza thamani kwenye zao la chai kwa ajili ya kuuza kwenye soko la nje na kwenye viwanda vya kuchanganya na kufunga chai kwenye vikasha. Alisema kampuni hiyo iliomba leseni ya kuchanganya na kufunga chai kwenye vikasha ikiwa ni hatua ya pili ya kuongeza thamani kwenye zao la chai.

"Kutokana na sheria ya chai, ilitakiwa kuanzisha kampuni tanzu kwa ajili ya kutekeleza shughuli hiyo kama ambavyo imeanishwa na sheria husika ya kuchanganya na kufunga chai kwenye vikasha,"alisema.

Manyanya alisema kwa utaratibu wa sasa, hakuna kampuni ambayo imezuiliwa kuchanganya na kufungasha chai kupitia kampuni tanzu.