Kiwanda cha manukato kuanzishwa Zanzibar


Na Thabit Hamidu, Zanzibar.

Waziri wa Biashara na Viwanda Zanzibar Balozi Amina Salum Ali amesema Zanzibar inatarajia kuanzisha kiwanda kikubwa cha kisasa cha Manukato ambacho kitakuwa na alama maalum ya Zanzibar (BRAND).

Amesema alama hiyo maalumu (BRAND) itakayokuwa katika bidhaa zitakazozalishwa kiwandani humo ni kwa ajili ya kuitangaza Zanzibar katika soko la kimataifa.

Kauli hiyo ameitoa jana  katika Ukumbi wa Baraza la wawakilishi Chukwani nje kidogo ya mji wa Zanzibar wakati akijibu swali la nyongeza la mwakilishi wa nafasi ya wanawake Saada Ramadhani  Mwenda  alietaka kujua mpango wa Serikali katika kuanzisha kiwanda cha Manukato na kupunguza kuagiza kwa wingi bidhaa hizo.

Akijibu swali la Mwakilishi huyo Waziri Balozi Amina alisema Serikali imejipanga kuanzisha kiwanda hicho na kupunguza gharama na kiwango cha uagizaji wa manukato kutoka Nchi mbali mbali.

“Kama mnavyojua Zanzibar ni kisiwa cha Manukato na miaka yote hii manukato yanafanywa na wajasiriamali sasa imefika wakati Zanzibar kuwa na kiwanda kikubwa na cha kisasa cha manukato ambacho kitakuwa na brand ya Zanzibar”Alisema Waziri Balozi Amina Salum Ali.

Balozi Amina alisema kwa hatua ya mwanzo ya kuanzisha kiwanda hicho kikubwa cha manukato Serikali kupitia Wizara  yake tayari wameanza kufanya tafiti mbali mbali  za Majani ambayo yanaweza kutumika katika kutengeneza manukato hayo.

“Hapo nyuma tulikuwa na kiwanda cha manukato kule mahonda, tumepokea wageni kutoka misri na kuwatembeza kiwandi pale na kutushauri kuwa tuoteshe baadhi ya majani ili kuanza na kuzalisha manuka mbai mbali”aliongeza kusema Balozi Amina.

Katika Malezo yake Balozi alisema kuwa Serikali inaendelea na hatua mbalimbali katika kuwashajihisha wawekezaji wa ndani na nje kuja kuwekeza katika viwanda vidogo na vikubwa vya manukato.