Makosa yanayofanywa na wajasiriamali wengi


Wajasiriamali wengi wamekuwa wanafanaya makosa Fulani fualani yanayowafanya washindwe kusonga mbele katika sula la kupata mafanaikio. Baadhi ya makosa hayo ni pamoja na;

Kupuuza maoni ya wateja
“Mteja ni mfalme”; je unalifahamu hili? Wajasiriamali wengi hupuuzia maoni ya wateja bila kujua kuwa maoni ya wateja ndiyo huwawezesha kujirekebisha na kuweza kuwapa wateja wao kile wanachokihitaji. Kosa hili lisiposhughulikiwa litakupotezea kiasi kikubwa cha wateja na kuleta matokeo mabaya kwenye biashara au mradi wako.

Kuacha fursa zipite
Wajasiriamali wengi hupenda kungojea mazingira yawe mazuri bila hata kujali fursa zinazopotea. Ni dhahiri kuwa hakuna mtu atakaye kutengenezea mazingira unayotaka; ukiona fursa itumie na mambo yatakaa vyema mbele ya safari. Inawezekana fursa unayoiona leo kesho isiwepo tena.

Kukataa ushauri wa kitaalamu
Kila kitu kizuri kinahitaji maarifa stahiki ili kiweze kutokea. Ni dhahiri kuwa wajasiriamali wengi wanafanya kosa la kupuuza ushauri wa kitaalamu katika kazi zao kwa kuona kuwa hauna nafasi. Kwa mfano kama unafuga kuku au unalima mazao fulani kwanini usimwite mtaalamu wa kilimo au mifugo ili akushauri? Ni dhahiri kuwa ukipata ushauri wa kitaalamu utakuwa mwenye tija zaidi.

Kutokwenda na soko linavyotaka
Mjasiriamali mzuri ni yule anayefahamu kuwa kwa sasa soko linataka nini. Ni lazima uweze kuepuka kosa la kutokutazama mahitaji ya soko, ili uhakikishe mauzo ya bidhaa au huduma yako hayaathiriki. Kwa mfano zamani watu walinunua zaidi kuku walio hai, lakini leo soko la kuku waliochinjwa ni kubwa pia; kwanini wewe bado unauza tu kuku walio hai? Ni dhahiri ukitazama mfano huu utaona jinsi kosa hili linavyowaathiri wajasiriamali wengi katika maeneo mbalimbali.

Kushindwa kubaini wateja lengwa
Ni lazima wewe kama mjasiriamali uwabaini wateja wako ili huduma au bidhaa yako iuzike. Kwa mfano umetengeneza dawa ya kuua mbu, kisha unaiuza mikoa ya baridi badala ya mikoa yenye joto (kwenye mbu wengi); ni dhahiri kuwa hutoweza kupata wateja wa bidhaa yako sawa sawa. Chukua hatua leo watafute na uwafuate wateja sahihi wa huduma au mradi unaoufanya.

Mbinu duni za masoko
Maswala ya masoko ni taaluma kamili ambayo watu hujifunza katika shule na vyuo mbalimbali. Hivyo ni muhimu wewe kama mjasiriamali kutokupuuzia taaluma hii kwani ndiyo itakayokuwezesha kubaini njia bora na sahihi za kuuza huduma au bidhaa yako. Hakikisha mbinu za masoko unazifahamu vyema tena zinaendana na soko husika la bidhaa yako. Hakikisha pia mbinu zako zinabadilika kulingana na mazingira na hali ya soko.

Maarifa sahihi ni msingi wa kufanya vitu kwa ubora. Ni dhahiri kuwa makosa mengi yaliyoelezwa hapa yanatokana na ukosefu wa maarifa stahiki ya ujasiriamali. Nakushauri ujifunze kila siku ili kupanua uwezo na uzoefu wako wa kiujasiriamali. Pia usisahau kuweka kwenye matendo yale yote unayojifunza.