Mapambano dhidi ya UKIMWI yaendelea


Na. Amiri kilagalila-Njombe

Wakijadili mafanikio na changamoto za mapambano dhidi ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI,  Wadau na Asasi zinazojishughulisha na   mapambano hayo katika Halmashauri ya Mji Njombe  wameazimia kwa pamoja kuendelea kuweka jitihada katika  kuelimisha jamii kuhusu janga la UKIMWI na kuitaka jamii kubadilika.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha ya Mapambano dhidi  ya UKIMWI  katika Halmashauri ya Mji  Njombe, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Thadei Luoga alisema kuwa elimu zaidi iendelee kutolewa hususani kwa wanafunzi mashuleni ili kuweza kunusuru kizazi cha sasa na kijacho dhidi ya janga hili.

“Tuna jukumu kubwa la kuendelea kuielimisha jamii bila kukata tamaa. Hatuna budi kama wadau kutumia fursa ya majukwaa  mbalimbali kuweza kuzungumzia swala la UKIMWI hususani katika Halmashauri yetu ambayo iko ndani ya Mkoa wa Njombe na unaongoza Kitaifa kwa kuwa na  asilimia 11.4. Katika sekta ya elimu tuone ni kwa namna gani tunaweza kuandaa nyimbo za mapambano dhidi ya UKIMWI wanafunzi wakawa wanaimba kama vile wanavyoimba nyimbo za shule hii itasaidi  kukuza uelewa na kutengeneza kizazi kitakachoweza kujikinga na janga la UKIMWI.”Alisema Luoga.

Aidha Luoga amewataka Maafisa Elimu, Waratibu Elimu, Wakuu wa Shule na Waalimu Wakuu kutojiweka pembeni kwenye mapambano haya kwani wapo wanafunzi wengi ambao ni walengwa (wanaishi na VVU)  na wanapaswa kuangaliwa kwa kipekee  kwani Uwingi wa VVU kwa wanafunzi hawa umeonekana kuwa wa juu zaidi ambapo kiwango kinachotakiwa (copies kuwa juu ya 1000), kuepuka unyanyapaa lakini pia waalimu ndio wenye jukumu la kuhakikisha ratiba zinakuwa rafiki kwa wanafunzi wanaoenda kuchukua dawa lakini pia kwenye usimamizi wa matumizi ya dawa hizo haswa kwa wale waliopo shule za bweni.

Silverius  Kesanta mwakilishi kutoka shirika la Jhpiego AIDS Free ambalo linajihusisha na utoaji wa huduma za tohara ya hiari kwa wanaume ambaye  kwa upande wake alisema kuwa changamoto kubwa  inayowakabili ni uwepo wa watoa huduma wachache waliopatiwa mafunzo ya utoaji tohara ambao wamekuwa wakichukuliwa na Wizara kwenda kufanya kazi katika Mikoa mingine inayoendesha kampeni za Tohara pasipo na taarifa na hivyo kusitisha huduma katika vituo vyao vya kazi jambo linalopeleka kukoma kwa huduma katika maeneo yao ya awali.

Mwakilishi wa shirika la JSI Clarence Mkoba  amesema kuwa miongoni mwa mafanikio waliyoweza kufikia ni kuzijengea uwezo kamati za Kuthibiti UKIMWI kuhusu mwongozo wa usimamizi wa kamati hizo ambapo katika Halmashauri ya Mji Njombe wamefanikiwa kujengea uwezo Kata 05  kati ya 13 ambapo kumekuwa na mafanikio chanya.

Kwa upande wake  Mratibu wa UKIMWI Halmashauri ya Mji Njombe Daniel Mwasongwe amesema kuwa warsha hizo ambazo zimekuwa zikifanyika kila kipindi cha robo mwaka zimekuwa na manufaa makubwa kwani zimesaidia upatikanaji wa taarifa za shughuli za utekelezaji wa Asasi.

“Kupitia warsha hizi tumekuwa tukibadilishana uzoefu,kupata taarifa za shughuli za utekelezaji  na kuweza kutatua changamoto kwa pamoja kwa jinsi kila mtu anavyofanya kazi katika kwenye mipaka yake. Usimamizi wa rasilimali kwa upande wa Halmashauri  unakuwa mzuri kwani kama kazi ipo kwenye mpango na inafanywa na Asasi fulani hakuna haja ya kutumia rasilimali kufanya kazi ambayo inafanywa na mdau mwingine. Hii pia inasaidia kuepusha migongano ya kazi kufanywa na asasi zaidi ya moja.”Alisema Daniel.

Ikumbukwe kuwa dira ya Taifa ya mapambano dhidi ya UKIMWI Tanzania ni kuwa na jamii isiyokuwa na maambukizi mapya ya VVU,Wakati mkakati wa dunia kwenye masuala ya VVU na UKIMWI ni kuwa Ifikapo 2030,dunia nzima inatakiwa kufika sifuri tatu(3 zero) yaani Maambukizi mapya ya VVU-0,Vifo vitokanavyo na UKIMWI-0,Unyanyapaa na ubaguzi kwa WAVIU-(0) na malengo ya muda mfupi ikiwa Ifikapo 2020,dunia nzima inatakiwa kufikai asilimia tisini tatu (90%,90%90%),yaani 90% ya watu wote walioambukizwa VVU wajue hali zao (Wapime VVU), 90% ya watu waliokutwa na VVU wajiunge na huduma ART (Waanze  kutumia dawa), 90% ya wanaotumia dawa wawe wamefikia hali ya kufubaza VVU(Viral Load Seppression).