Mfanyabiashara anyang’anywa maeneo Longido


Mfanyabiashara maarufu wa Jijini Arusha, Philemon Monaban amenyang’anywa maeneo yake yaliopo wilayani Longido ambayo anadaiwa kuyavamia kinyume na utaratibu, baada ya tume  iliyoundwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Frank Mwaisumbe kubaini hilo.

Tume hiyo iliundwa kufuatilia mgogoro wa ardhi uliodumu kwa muda mrefu, kati ya mfanyabiashara huyo na Ismail Kilas, Jackline Bendera,Aisha Mkwawa na Jane Sylvesterna.

Akithibitisha tukio hilo jana wilayani humo, Katibu Tawala Wilaya ya Longido, Toba Nguvila, alisema Tume iliazimia chini ya Mkuu wa Wilayakuwa Mollel (Monaban), kuachia hayo maeneo ya watu hao sababu aliyavamia bila kufuata sheria.

Tume hiyo ilihusisha wataalamu mbalimbali kutoka Ofisi ya Mwanasheria, Ardhi, Mkurugenzi Mtendaji, Takukuru, Usalama wa Taifa, Jeshi la Polisi, Katibu Tarafa wa Longido, Ofisa Mtendaji Kata ya Kimokouwa, Mtendaji wa Kijiji cha Eworendeke na Mwenyekiti wa Kijiji cha Eworendeke.

Alisema muongozo uliotumika katika kuchunguza mgogoro huo ni kupitia hadidu tatu za rejea ambazo walipitia mikataba ya umiliki,kujiridhisha kama kanuni za umiliki kwa pande zote mbili zilifuatwa na pamoja na mambo mengine, ambayo kamati ingeona ni vyema kushauri katika mgogoro huo ili haki itendeke.

Hata hivyo, alisema tume ilitembelea eneo la mgogoro na kuwahoji watu muhimu, wakiwamo wahusika wa mgogoro, mashahidi wao, viongozi wa serikali ya kijiji husika, pamoja na wauzaji wa maeneo husika, hivyo watu 19 walifika mbele ya kamati kuhojiwa.

Alisema Machi Mosi, mwaka huu, kamati iliwasilisha matokeo ya uchunguzi kwa kamati ya Usalama wilaya na ilipofika Machi 21, pandezote mbili ziliitwa na kusomewa mashtaka pamoja na mapendekezo ya kamati, Mkuu wa Wilaya alikubaliana na mapendekezo sita kati ya nane.

“Kamati ilipendekeza kuwa, viwanja namba 143E ni cha Aisha Mkwawa, 144E cha Jane Sylvester, 145E cha Jackline Bendera na 97E,99E na 101Eapewe Ismail kilas, na hii ni baada ya kamati kubaini kuwa viwanja hivyo, ni mali ya wananchi hao,” alisema.

Pia kamati ilipendekeza Kilas aonyeshwe eneo la kujenga darasa ili alijenge kwa haraka kama walivyokubaliana na kijiji.

Kilas alisema alipewa viwanja na Serikali ya Kijiji cha Eworendeke mwaka 2008 kwa makubaliano ya ujenzi wa maegesho ya magari."Nilipewa kiwanja plot namba tatu na kijiji, lakini waliniambia nijenge darasa moja katika kitongoji cha matiani, nilikubali kufanyahivyo na nikakabidhiwa hati ya umiliki wa kijiji hicho," alisema.

Alisema, hakufanikiwa kujenga darasa hilo kutokana na mvutano baina ya kitongoji cha Matiani na Losoiti, kwa kutaka kila mmoja darasa hilo lijengwe kwake.

"Baada ya kutokea mvutano baina ya vitongoji hivyo, serikali ya kijiji iliniandikia barua ya kusitisha ujenzi huo hadi pale watakapo azimia darasa hilo lijengwe wapi," alidai.

Alidai mwaka 2012, Monaban alivamia eneo hilo, akiwa na askari polisi wenye silaha za moto na kuweka uzio kwa kudai kuwa eneo hilo ni mali yake.Alisema aliwasiliana na serikali ya kijiji baada ya kutokea hali hiyo na kijiji kilikanusha kumpa Monaban kiwanja hicho.Alidai kuwa, aliwasilisha uonevu huo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Juma Mhina, pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe na ofisi hizo ziliunda tume ya kuchunguza jambo hilo.

Alidai kuwa, baada ya tume kutoa maamuzi ya wao kurejesheshewa maeneo yao kutoka katika mikono ya Mollel alipokea notisiya siku 30 ya kufunguliwa shauri la madai mahakamani dhidi yao kwa madai ya kuvamia mashamba.

Mtendaji wa Kijiji cha Eworendeke, Ally Abed, alisema, ni kweli eneo lenye mgogoro ni mali ya Ismail na amekuta mikhutasari inayoonyesha kijiji kilimpatia eneo hilo.