https://monetag.com/?ref_id=TTIb Mizani 14 Njombe yakutwa na changamoto | Muungwana BLOG

Mizani 14 Njombe yakutwa na changamoto



Na Amiri kilagalila-Njombe

Meneja wa wakala wa vipimo mkoani Njombe Gasper Matiku amezitaka hospitali mbalimbali mkoani Njombe kuhakikisha kuwa mizani wanayoitumia katika hhughuli zao za matibabu zinafanyiwa marekebisho ya mara kwa mara ili kuepuka mizani hiyo kudanganya katika utoaji taarifa za wagonjwa na kuathiri matibabu yao.

Ikiwa ni wiki ya vipimo Duniani wakala wa vipimo Mkoani Njombe wametembelea na kufanya ukaguzi katika hospital ya rufaa Kibena pamoja na kituo cha afya Njombe mjini ambapo wamebaini kuwapo kwa mizani 14 yenye changamoto kati ya 26 iliyokaguliwa.

Mara baada ya kubaini kuwepo kwa mizani yenye changamoto Maneja wa wakala wa vipimo amezitaka Hospital na vituo vya afya pamoja na Zahanati kuwa na utaratibu wa kutenga fedha kwaajili ya matengenezo ya mizani hiyo pindi ikiharibiki.

"kwa hiyo tunawashauri ni vizuri sasa wakatenga bajeti kila mwaka kwa ajili ya kuona hizi mizani zisitumike tu bila kufanya service kwa sababu mizani ni kama mashine inavyotumika usahihi wake unaweza kupotea,kwasababu kuna parts ambazo kulingana na matumizi zinakuwa zinalika"alisema Gasper matiku

Shela Myemba ni Muuguzi msaidizi katika kituo cha afya Njombe mjini ameuomba wakala wa vipimo kuendelea kuwatembelea ili kubaini changamoto walizonazo katika masuala ya vipimo.

Kaimu Mganga Mfawidhi katika Hospitali ya Rufaa Kibena Dr Barnaba Baraka ametaja madhara ya kutumia mizani mibovu.

"katika swala zima la kutoa dawa kwasababu dawa zinatolewa kutokana na uzito unaweza ukatoa dawa ambazo sio sahihi,na kwa mizani ambayo imebainika kuwa na shida hiyo kwanza haitatumika mpaka pale itakapofanyiwa marekebisho na kujiridhisha kuwa ipo sawa"alisema dk.Barnaba