Nape awasha moto Bungeni swala la korosho, amtaja CAG


Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye amesema hali ya wakulima wa Korosho hivi sasa ni mbaya licha ya nia njema ya Rais kutaka wakulima wa zao hilo kulipwa.

Ameeleza kuwa zoezi hilo limetawaliwa na dhuluma pamoja na rushwa, huku akibainisha kuwa zaidi ya wakulima 1181 bado mpaka sasa katika jimbo la Mtama hawajalipwa pesa zao.

Nape ameishauri Serikali kumruhusu Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, kwenda kufanya ukaguzi katika zoezi hilo ili kuubaini ukweli, huku akitaka wale wote waliohusika katika mchakato wa uuzaji Korosho wawajibishwe kutokana na dhuluma wanayodaiwa kuifanya kwa wananchi wa Mtwara.

Naye Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini amemshauri Spika wa Bunge kuunda kamati ya wabunge wachache, kukagua maghala ya kuhifadhi Korosho, lengo likiwa ni kubaini Korosho nzima na zilizooza kutokana taarifa kuwa zaidi ya asilimia 30 ya Korosho zimeoza.