RC Dodoma awataka watendaji kuandika barua za kujieleza


Na.Enock Magali,Dodoma

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Chamwino Athuman Masasi,kuandika barua ya kujieleza kuwa ni kwanini ameshindwa kufikia lengo la ugawaji wa vitambulisho kwa wajasiriamali vilivyotolewa na Mh.Rais Dkt.John Pombe Magufuli.

Dkt Mahenge amefanya ziara katika wilaya ya Mpwapwa na Chamwino ambapo amekagua idadi ya wajasiriamali waliokwisha pata vitambulisho sambamba na kuendesha zoezi la ugawaji wa vitambulisho hivyo kwa wakuu wa idara wa Halmashauri hizo.

Akiwa wilayani Chamwino Dkt.Mahenge amesikitishwa na hali ya uendeshaji wa zoezi hilo kwani kati ya vitambulisho 800 walivyo pewa katika awamu ya pili wamekwisha uza 57 pekee sawa na asilimia moja tu,jambo lililopelekea kutoa maagizo kwa watendaji wa Kata pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuandika barua za kujieleza.

Aidha akiwa wilayani Mpwapwa Dkt.Mahenge amewataka watendaji kutowatoza ushuru wa aina yoyote wajasiriamali walio kata vitambulisho huku akiendelea kusisitiza suala la usafi lifanyike kwa maelewano ya wafanyabiashara na viongozi wao.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Mh.Jabir Shekhmweri ameahidi kuyatekeleza maagizo ya Mkuu wa Mkoa huku akisema kuwa kuanzia kesho ataendesha Oparesheni ya kukagua wafanya biashara wenye vitambulisho na kama mtu asipokuwa nacho basi atalazimika kufunga biashara.

Mkuu wa Mkoa bado anaendelea na ziara yake katika wilaya mbalimbali za mkoa huu kwa lengo la kugawa vitambulisho hivyo kwa wakuu wa Idara na kufanya uhamasishaji wa wajasiriamali kuwa na vitambulisho.