https://monetag.com/?ref_id=TTIb Serikali yajiwekea mkakati wa kupanda miti Mil. 280 nchi nzima | Muungwana BLOG

Serikali yajiwekea mkakati wa kupanda miti Mil. 280 nchi nzima


Serikali imeweka mkakati wa kupanda miti Milioni 280 kati ya mwaka 2016/20 katika maeneo mbalimbali nchini.

Kauli hiyo aliitoa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Costantino Kanyasu wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Same, Magharibi, Nagenjwa Kaboyoka (Chadema).

Mbunge huyo alitaka kujua kama serikali inaweza kwenda kushauriana na wananchi wa vijiji jimboni kwake ili kutenga maeneo kwa ajili ya kuanzisha misitu ya vijiji.

Kanyasu alisema serikali haina kipingamizi kushirikiana na vijiji katika kutenga maeneo kwa ajili ya kuanzisha misitu ya kijiji lakini mara nyingi baadhi ya wananchi wamekuwa wakifanya hivyo na baadaye wanageuka na kudai maeneo yao.

Alisisitiza kuwa endapo wananchi wa jimbo na mbunge huyo wapo tayari, basi serikali itashirikiana nao. Akijibu swali la msingi la Kaboyoka aliyetaka kujua serikali ipo tayari kuanzisha mradi wa utunzaji mazingira katika kata za Bendera, Kihurio, Ndungu na Maore ili kuhifadhi mazingira. Kanyasu alisema wilaya ya Same kiikolojia na kijiografia imegawanyika katika kanda kuu mbili yaani ukanda wa milima ambao hali yake ya hewa ni nzuri ukilinganisha na ukanda wa tambarare ambapo hali ya hewa ni ukame.