Ujenzi wa vyoo shule ya msingi mapambano jijini Mbeya ni kitendawili


Siku moja baada ya kikao cha ndani cha wananchi na wajumbe wa kamati ya maendeleo ya kata (WDC) kuketi na kutaka kupata  taarifa ya mapato na matumizi ya fedha zilizotolewa za ujenzi wa choo shule ya Msingi Mapambano kutoka kwa mtendaji wa kata ya Iyela Anna Sipalika,hii Leo mtendaji huyo amesema ana wajibu wa kutoa taarifa kwa mkurugenzi na si vinginevyo.

Awali kikao hicho kilichoketi 18 May,2018 na kuhudhuriwa pia na mdau wa maendeleo Ndele Mwaselela na diwani wa kata ya Iyela kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Charles Mkela,kilitaka kupata taarifa hiyo ili kufahamu endapo fedha zilizotolewa na mfuko wa jimbo shilingi milioni 10 zimeisha ama bado ili mdau huyo amalizie ujenzi ambao umeonekana kuchukua muda mrefu pasipo kukamilika.

Wajumbe wa kikao hicho wamesema walimtaka Afisa Mtendaji kata ya Iyela kutoa taarifa na kudai kuwa ni mara nne amekuwa akitoa sababu ambazo sio msingi za kutohudhuria vikao,hivyo inaonesha kuna mgogoro ambao unaendelea na unasababisha ujenzi kutokamilika na taarifa ya mapato na matumizi kutotolewa.

Disemba,2018 mbunge wa jimbo la Mbeya mjini Joseph Mbilinyi(CHADEMA) alitembelea shuleni hapo na kukuta changamoto ya vyoo ambayo imedumu kwa miaka 10 na kuahidi kulishughulikia ambapo fedha zilitolewa kiasi cha shilingi milioni 10,ambazo mpaka sasa hazijamaliza ujenzi na kuwafanya wanafunzi wajisaidie katika mazingira yanayozunguka shule hiyo kutokana na ubovu wa vyoo vya awali.

Akizungumza na mtandao huu, diwani wa kata ya Iyela,Charles Mkela,amesema kuwa amesikitishwa na taarifa ambazo zimekua zikitolewa na watu tofauti juu ya fedha hizo za mfuko wa jimbo za ukamilishaji wa ujenzi wa vyoo hivyo na kuongeza kuwa ujenzi unaendelea na utakamilika hivi karibuni.

Baada ya kuwepo kwa taarifa ya kusua sua  kwa ujenzi huo,mdau wa maendeleo Ndele Mwaselela,amesema yupo tayari kumalizia kujenga vyoo hivyo endapo atapata taarifa kuwa fedha iliyotolewa na mfuko wa Jimbo imemalizika ama la!ili kufikia mwezi Julai vyoo viwe vimekamilika na watoto waanze kuvitumia.