Upelelezi kesi ya kigogo TAKUKURU haujakamilika


Serikali imesema upelelezi wa kesi inayomkabili aliyekuwa mkurugenzi wa mipango na ufuatiliaji na tathimini wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) Kulthum Mansoor anayekabiliwa na mashtaka nane ikiwemo la utakatishaji fedha kiasi cha shilingi bilioni moja na milioni mia nne bado haujakamilika.

Wakili wa serikali Tully Helela ameiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa shauri hilo lilifika mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa kwa kuwa upelelezi bado unaendelea na kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya shauri la kesi hiyo kufika mahakamani hapo.

Kufuatia maelezo ya upande wa mashtaka hakimu mkazi mfawidhi, Kelvin Mhina ameiahirisha kesi hiyo hadi juni nne mwaka huu itakapokuja mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa na mshtakiwa huyo amerudishwa rumande.

Katika kesi ya msingi mshtakiwa huyo anakabiliwa na mashtaka ya kughushi tarehe tofauti kati ya januari 2013 hadi mei 2018 akiwa makao makuu ya TAKUKURU yaliyopo jijini Dar es Salaam ambapo alitoa barua ya ofa ikionyesha barua hiyo imetoka katika halmashauri ya wilaya ya Bagamoyo huku akifahamu kufanya hivyo ni kosa la kisheria.

Katika kosa lingine inadaiwa mshtakiwa huyo alijipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kiasi cha shilingi milioni tano kutoka kwa mtumishi wa TAKUKURU Alex Mavika kama malipo ya kiwanja kilichopo kijiji cha ukuni wilaya ya Bagamoyo huku akionyesha yeye ni mmiliki wakati akijua ni uongo.

Aidha katika kosa la utakatishaji fedha inadaiwa kati ya tarehe tofauti januari mwaka 2013 na mei 2018 akiwa eneo la Upanga jijini Dar es Salaam mshtakiwa alijipatia shilingi bilioni moja na milioni mia nne huku akijua fedha hizi ni za makosa mengine.