Viongozi watakiwa kuwa wanyenyekevu na hofu ya Mungu


Na Alphonce kusaga.

Mwenyekiti wa jumuiya ya wanawake UWT mkoa wa Arusha Yasmini Bachu amewataka viongozi waliopewa dhamana kuwa wanyenyekevu na hofu ya Mungu lakini wasiache kuwa wakali katika kukemea mambo ya Hovyo.

Akizungumza na wanawake wa Jumuiya ya Wanawake kutoka kata tano za Muivaro, Olorieni, Moshono, Kimandolu na Baraza Jiji la Arusha, Bachu amesema kuwa kila kiongozi mwenye nafasi anatakiwa kutumikia wananchi kwa Moyo wote kwasababu ndiyo jambo la msingi ambalo wananchi wanalihitaji.

Hata Hivyo amesema katika kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wanawake wanatakiwa kujitokeza kugombea nafasi za uenyeviti wa Serikali za Mitaa na kuwa mstari wa mbele kuchukua fomu za Kugombea na wasisubiri nafasi za ujumbe wa Serikali za Mitaa

Amesema kupitia nguvu ya wanawake ambao ni jeshi kubwa wanategemea kushinda kata zote 161 za mkoa wa Arusha hivyo watapatikana wawakilishi wa viti maalum vingi vinavyotokana na wanawake kwa kuwa uongozi hauna hati miliki.

Amesisitiza kuwa wao kama wanawake wanatakiwa kuchagua pia viongozi ambao wanaendana na taswira ya Chama cha Mapinduzi na ambao watakuwa wanashiriki pamoja katika shida za wananchi.

Ameongeza mwanamke ni kiongozi tangu kuzaliwa kwasababu majukumu ya uongozi yameanzia katika familia zao hivyo inaweza kuwa kipimo tosha cha uongozi na kujipima unavyokubalika katika jamii yako.