https://monetag.com/?ref_id=TTIb Vipimo vya Dengue vyaongezwa | Muungwana BLOG

Vipimo vya Dengue vyaongezwa


Serikali imesema inaendelea kuimarisha upatikanaji wa vipimo vya homa ya dengue katika vituo vyake vya kutolea huduma katika maeneo yaliyoathirika zaidi.

Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Muhammad Kambi alisema Dar es Salaam kuwa kuna vipimo 43 (kits) kwenye Maabara ya Taifa vyenye uwezo wa kuhudumia wagonjwa 430.

Alisema vipimo vingine 200 vyenye uwezo wa kuhudumia wagonjwa 2,000, vitasambazwa na Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kwenye Vituo vya Afya vya serikali. Katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya vipimo kwa urahisi, Profesa Kambi alisema serikali imeagiza vipimo vingine 3,000 vya kupima wagonjwa 30,000.

Alisema kati ya hivyo, vipimo 200 kwa ajili ya kupima wagonjwa 2,000 vitawasili hivi karibuni na kusambazwa kwenye vituo vya umma mkoani Dar es Salaam na mikoa mingine. Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha vituo vya umma vinakuwa na vipimo vya kutosha kwa ajili ya kuwahudumia wananchi waliokumbwa na ugonjwa huo.

"Mpaka sasa, ugonjwa huu hauna chanjo wala tiba ya moja kwa moja, niwatahadhirishe wanaotoa taarifa za upotoshaji kuhusu tiba ya ugonjwa huu kupitia mitandao ya kijamii,"alieleza Profesa Kambi.

Vituo vilivyotajwa kupima homa ya dengue mkoani Dar es Salaam ni Muhimbili, Maabara Kuu Muhimbili, Amana, Temeke, Mwananyamala, Sinza, Vijibweni, Mnazi Mmoja, Lugalo, Mbagala, FFU Ukonga, wakati mkoani Tanga ni Bombo na Horohoro, vingine ni Tumbi, Mkuranga, Utete Rufiji, Mafia, Morogoro na Manyara.

Hali ya ugonjwa ilivyo Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Serikali, homa ya dengue imezidi kuongezeka kwa kuwa kuna jumla ya wagonjwa 1,901 waliothibitishwa kupitia vipimo vya maabara, kuwa wana virusi au walikwishapata ugonjwa wa dengue katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Mei 15 mwaka huu. Alisema takwimu za ugonjwa huo katika kipindi cha siku tisa tangu watoe tamko lao wiki iliyopita, zinaonesha kwamba kuna ongezeko la wagonjwa wapya 674 sawa na wastani wa wagonjwa 75 kila siku. Profesa Kambi alisema ongezeko hilo, limetokana na kuongezeka kwa uelewa wa wananchi kuhusu ugonjwa huo na kujitokeza kupata huduma za uchunguzi katika vituo vya afya.

"Kati ya wagonjwa 1,901, wagonjwa 1,809 ni kutoka Dar es Salaam, 89 Tanga, Singida 1, Kilimanjaro 1 na Pwani 1; wagonjwa waliopatikana katika mikoa ya Kilimanjaro na Pwani wote walitokea Dar es Salaam na mpaka sasa hakuna vifo,"alieleza Profesa Kambi.

Hali ilivyo Dar Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yudas Ndungile, alisema kata 20 za mkoa wake ndizo zilizoathirika zaidi kwa kuwa na idadi ya wagonjwa wanaozidi 25. Alitaja kata hizo kuwa ni Ilala yenye wagonjwa 235, Upanga (87), Kisutu (86), Kariakoo (79), Sinza (223), Mbezi (78), Kimara (65), Masaki (56) na Msasani (50).</p>

"Kata zingine ni Wazo yenye wagonjwa 49, Kinondoni (45), Mikocheni (40), Gerezani (40), Tabata (41), Ukonga (27), Mbezi Beach (37), Tandale (38), Kijitonyama (34), Mwenge (28) na Tegeta (27), hivyo manispaa zote za mkoa huo zimekumbwa na homa ya Dengue kwa kuwa kata zingine zina wagonjwa chini ya 25. Kutokana na kasi ya homa hiyo, Ndungile alisema kuna taratibu zinakamilishwa ili kupata mashine ya kuweza kupulizia dawa kutokea angani ili kuuwa mbu hao katika maeneo mbalimbali ya jiji na makazi ya watu.

Dalili za ugonjwa Dalili za homa ya Dengue zimetajwa kuwa ni kuugua homa ya ghafla, kuumwa kichwa hasa sehemu za macho, maumivu ya viungo na uchovu na dalili hizo hujitokeza kati ya siku tatu hadi 14 tangu mtu alipoambukizwa virusi vya homa hiyo. Mganga Mkuu wa Serikali alisema wakati mwingine dalili za ugonjwa huo hufanana na za ugonjwa wa malaria.