https://monetag.com/?ref_id=TTIb Watendaji waonywa vibali vya kusafirishia mifugo mnadani | Muungwana BLOG

Watendaji waonywa vibali vya kusafirishia mifugo mnadani


Na Timothy Itembe, Mara.

Jeshi la polisi limewataka  watendaji wa mitaaa,vijiji na kata  kuwa makini pindi wanapokuwa wanatoa vibali kwa wafanyabiashara wa mifugo wanapohitaji  vibali hivyo kwaajili ya kusafirisha mifugo yao kwenda mnadani kuuzwa.

Mkuu wa kikosi cha kupambanba na wizi wa mifugo,Tarime/Rorya,Ally Manyamba alisema juzi katika kikao cha madiwani cha kata kuwa kuna baadhi ya watendaji katika maeneo wanayoongoza wanatoa vibali vya kusafirisha mifugo kwenda mnadani kuuzwa ambapo hawawi makini na badala yake wanatoa vibali hivyo hata kwa majambazi.

Manyamba aliongeza kuwa wimbi la wizi wa mifugo kwa Tarime/Rorya linashika kasi kwa kuwa jamii iliyopo imelifanya jambo hilo kama jadi yao na hawataki kumsema mwizi badala yake wanamkumbatia.

Sisi Jeshi la polisi tunahakikisha kuwa tunapambana na wimbi hilo kwa kutumia njia mbadala ili kuhakikisha kuwa wananchi wanaondokana na kero hiyo kwa kuwa Serikali yetu haikubaliani na matukio ya kiuhalifu inataka wananchi wake wakae salama huku wakiendelea na shuguli zao za kila siku za kujenga Taifa.

Pia Manyamba alitumia nafasi hiyo kuwataka madiwani katika maeneo wanayoongoza kwenda kutoa elimu ya kupinga vitendo vya wizi wa mifugo kwa wapiga kura wao ili  kuacha wizi wa mifugo kwani kipindi hiki wizi hauna nafasi ambapo pia aliwatahadharisha watendaji kutoa vibali hivyo kwa umakini na kila mfugo kuwa na kibali  chake badala ya kuunganisha mifugo mingi ndani ya kibali kimoja.

Kwa upande wake mwenyekiti wa halmashauri ya Mji wa Tarime,Khamisi Nyanswi aliwataka madiwani wenzake pamoja na watendaji kwenda kufanya mikutano ya hadhara ya kuwabaini wezi wa mifugo kwa njia ya kupigiwa kura na wananchi.

"Mimi niwatake madiwani wenzangu pamoja na watendaji kwenda kufanya mikutano katika maeneo yanu ya kuwabaini wezi wa mifugo huku mkiwatumia wananchi kwa kuwapigia kura ya siri wezi wa mifugo na haiwezekani Mtu akapigiwa kura nyingi na wananchi kama siomwizi wa mifugo"alisema Nanswi.

Nyanswi aliongeza kuwa kuna haja Jeshi la polisi kufumba macho kidogo pindi wanaposikia kuwa wananchi wamekamata mwizi wa mifugo ili wananchi wenyewe wamsulubu kwanza kwani wezi hao wamesumbua mda mferu na kuwa wakikamatwa wanaachiwa kutokana na ushahidi kukosa mahakamani.