Waziri Mkuu mpya wa DR Congo aahidi kuimarisha usalama


Rais wa DR Congo, Felix Tshisekedi amemteua Sylvestre Ilunga Ilunkamba kuwa Waziri Mkuu, kuongoza serikali ya muungano kwa mujibu wa makubaliano ya kisiasa kati yake na rais wa zamani Joseph Kabila.

Ilunkamba ameaanza kazi leo na ameahidi kuboresha maisha ya wananchi na kurejesha usalama, katika nchi hiyo ambayo imekumbwa na matatizo makubwa ya kiusalama.

Waziri Mkuu huyu mpya ni mwanasiasa mkongwe nchini DR Congo na anatokea katika jimbo la Katanga, na katika uzoefu wake wa kuwa katika ulingo wa kisiasa kwa miaka 30, aliwahi kuwa mshauri wa rais wa zamani Mobutu Seseko.

Uteuzi huu umekuja baada ya majadiliano ya muda mrefu kati ya rais Tshisekedi na Kabila, kwa sababu kwa mujibu wa Katiba ya nchi hiyo, Waziri Mkuu anastahili kutoka kwenye chama chenye wabunge wengi wabunge.