Chama cha Walimu Tanzania kuanza kufanyia kazi ripoti ya CAG


Chama cha Walimu Tanzania (CWT), kimesema kinaifanyia kazi ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu matumizi ya mali na  fedha.

Chama hicho kupitia Bodi ya Wadhamini kimesema , kitaendelea kulinda na kutetea masilahi na  mali za walimu nchini.

Hayo yalielezwa jijini Dodoma na Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa CWT, Clement Mswanyama,  kwenye Mkutano wake na waandishi wa habari.

Mswanyama alikuwa  akitoa ufafanuzi kuhusu umiliki wa mali za CWT. Alitoa ufafanuzi  kuhusu majengo, mali za chama hicho na Benki ya Walimu (MCB) kutumiwa vibaya, pamoja na umiliki wa  Kampuni ya Teachers Development Company Ltd (TDCL).

Mswanyama alisema kwamba CWT itaendelea kulinda na kutetea mali za walimu nchini kwa kuhakikisha zinakuwa katika mikono salama.

Alisema kwa mujibu wa Katiba ya CWT toleo la sita la mwaka 2014, mali za chama zitaandikishwa kwa jina la Bodi ya Wadhamini, pia mikataba yote, hati na dhamana za fedha za chama zote zitamilikiwa kwa jina hilo na kuhifadhiwa kwa Katibu Mkuu wa CWT.

Mswanyama alisema wanaishukuru ofisi ya CAG kwa kufanya ukaguzi katika chama chao na kwamba wanaendelea kuyafanyia kazi mapendekezo ambayo yamependekezwa katika usimamizi wa fedha na mali.