Dkt. Shein aupongeza uongozi wa Makampuni ya Okan


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ameipongeza azma ya uongozi wa Makampuni ya Okan yenye makao makuu yake nchini Uturuki inayokusudia kujenga hospitali ya utibabu wa meno hapa Zanzibar.

Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipofanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Makampuni ya Okan ambaye pia, ni Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini wa Chuo Kikuu cha Okan kiliopo Istanbul nchini Uturuki akiwa amefuatana na Balozi wa Uturuki nchini Tanzania Ali Davutaglu.

Katika maelezo yake Rais Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar na Uturuki zina historia kubwa hali ambayo imepelekea hadi lugha ya Kiswahili kutohowa baadhi ya maneno kutoka katika lugha ya Kituruki.

Mbali na hayo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa Zanzibar na Uturuli zina uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu hali ambayo imeimarika kutokana na uongozi thabiti wa pande mbili hizo.

Akieleza kuhusu azma hiyo ya Makampuni ya Okan ya nchini Uturuki kuja kujenga hospitali ya meno pamoja na mradi mwengine wa upanuzi na vifaa kwa ajili ya Hospitali ya MnaziMmoja, Rais Dk. Shein alisema kuwa hilo ni jambo la busara na litasaidia kuimarisha sekta ya afya hapa nchini.

Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaiunga mkono miradi hiyo na iko tayari katika kushirikiana na Makampuni hayo makubwa ya nchini Uturuki katika kuianzisha  miradi hiyo mara tu baada ya kukamilika kwa taratibu na majadiliano baina ya pande mbili hizo.

Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa upande wake itaunda timu maalum na kukaa pamoja na timu ya Makampuni hayo ya Okan kwa lengo la kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa na linakwenda kwa kasi na kufikia azma iliyokusudiwa.

Aliongeza kuwa tayari Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Chuo chake Kikuu cha Zanzibar (SUZA) ina mpango wa kuanzisha masomo yanayohusiana na kada hiyo ya utibabu wa meno, hivyo itakuwa ni jambo la busara kwa Chuo Kikuu cha Okan kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ajili ya kuanzisha Hospitali hiyo.

Rais Dk. Shein pia, alieleza azma ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kujenga Hospitali katika eneo la Binguni, Wilaya ya Kati, Unguja na kutoa ushauri kwa uongozi huo kuwa ni jambo la busara iwapo ujenzi wa hospitali hiyo utafanyika katika eneo hilo lenye ukubwa za hekta 45 kutokana na nafasi kubwa iliyopo ikilinganisha na eneo la Hospitali ya MnaziMmoja.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein aliunga mkono azma ya uongozi huo wa Makampuni ya Okan ya kuekeza katika sekta ya utalii hapa nchini na kusema kuwa hatua hiyo ni miongoni mwa utekelezaji wa sekta alizozijadili katika mazungumzo aliyoyafanya wakati wa ziara yake nchini Uturuki mwaka 2011 alipokutana na Rais wa nchi hiyo wakati huo Rais Abdallah Gul.