https://monetag.com/?ref_id=TTIb Hatua muhimu za kuzingatia katika ufugaji wa kuku | Muungwana BLOG

Hatua muhimu za kuzingatia katika ufugaji wa kuku



Katika matunzo ya kuku wanaokua, hapa tunaangalia kuku wenye umri wa kuanzia miezi miwili hadi minne. Kuku hawa wenye umri huu wanatakiwa watunzwe vizuri ili wakusaidie kukupa mfugaji faida, vinginevyo ukishindwa hapa kutunza kuku wako vizuri basi usitegemee kupata faida kubwa.

1. Hatua ya 1, waweke kwenye banda kubwa.
Hatua hii inakuja kama walikua bado kwenye eneo la kulea vifaranga, wahamishe na uwapeleke kwenye banda kubwa. Kama banda ni hilo hilo moja, waondolee ‘hardboards’ ulizokuwa umetengea vifaranga, na waachie kwenye banda zima.

2. Hatua ya 2, wawekee bembea kwenye banda.
Ukumbuke kwamba kuku ni ndege, hivyo kuna wakati wanapenda kuwa juu. Hivyo ni muhimu kuwawekea bembea ili iwasaidie kufurahia maisha yao na kuwa huru zaidi. Hiyo itakuwa ni sehemu mojawapo ya kufanya zoezi.

3. Hatua ya 3,  weka matandazo safi.                                                                               
Hakikisha matandazo yasiwe na harufu kali au vumbi.  Hakikisha pia maji hayamwagiki bandani. Na Mara tu yakimwagika ondoa matandazo yaliyolowa na weka mapya. Pia ukumbuke kubadilisha matandazo mapema ili yasiweze kutoa halafu na kuleta magonjwa mengine yatakanayo na matandazo kurundikana.

4. Hatua ya 4, weka ratiba ya usafi.
Unaweza ukaweka ratiba ya usafi bandani na kwenye eneo la kuzunguka banda, angalau mara mbili kwa wiki. Tumia dawa ya V-RID kufanyia usafi na kupulizia dawa hewani. Hii itasaidia banda lako kubaki safi wakti wote na afya kwa kuku wako pia.

5. Hatua ya 5, wape kuku maji safi muda wote.
Pia unaweza kuwaongezea vitamin kwenye maji yao hasa kama wanafugwa ndani muda wote. unapowapa maji safi muda wote si rahisi sana kuweza kupata magonjwa yatokanayo na bakteria.

6. Hatua ya 6, wape chakula chenye virutubisho.
Usiwape kuku wako ilimradi tu chakula, wape kuku wako chakula chenye virutubisho vya kutosha. Unaweza ukaanza kuwapa ‘growers’ au aina nyingine ya chakula kizuri. Ukiwalisha kuku wako chakula duni, wanadumaa.

7. Hatua ya 7, rudia chanjo ya newcastle kwa wakati.
Hii unaweza kufanya yaani kila baada ya wiki 10 tangu walipochanjwa mara ya mwisho. Unaporudia chanjo inasaidia sana kuwafanya kuku wako wawe imara wakati wote na inakuwa ngumu kukutana na magonjwa.

8. Hatua ya 8, wape dawa ya minyoo.
Dawa ya minyoo unawapa kuku wakiwa na miezi miwili na rudia kila baada ya wiki 10. Ukishindwa kuwapa dawa hii basi tegemea kuokota kuku wengi ambao watakufa kutokana na kushambuliwa na minyoo.

9. Hatua ya 9, walishe majani na mboga mboga kwa wingi.
Unapowalisha kuku majani ya mboga mboga hiyo itawairishia miili yao kwa kuiongezea kinga dhidi ya magonjwa. Hata hivyo kama kuku wakilishwa majani ni rahisi pia kuweza kutaga vizuri inapofikia kipindi hicho.

10. Hatua ya 10, kama una eneo kubwa, wafungulie nje ili wazunguke zunguke.
Waache kuku wako wazunguke na waoge kwenye mchanga.  Kuzunguka zunguka na kuparua parua kunawafanya bize na kudonoana na kulana manyoya. Kuoga kwenye mchanga kunawafanya wawe safi na kama wana wadudu, wanaweza kuwaondoka.

11. Hatua ya 11, kuwa na mawasiliano ya karibu na daktari wa mifugo.
Mara tu uonapo dalili za ugonjwa, wasiliana na daktari wa mifugo kwa ushauri zaidi. Pia tafuta chanzo cha ugonjwa ili ukiondoe.

Mwisho wa somo letu la leo na tunaamini umejifunza kitu cha kukusaidia kuboresha ufugaji wako.