https://monetag.com/?ref_id=TTIb Hatuna nia ya kuwakomoa wananchi - Mkurugenzi wa BAWASA | Muungwana BLOG

Hatuna nia ya kuwakomoa wananchi - Mkurugenzi wa BAWASA



Na John Walter-Babati .

Mkurungenzi wa Mamlaka ya Maji safi na usafi wa mazingira Babati (BAWASA) Idd Msuya amewataka wananchi kuacha kulalamika kuhusu kupanda kwa bei ya maji kwa unit  kutokana na uhitaji mkubwa wa fedha za kuendelea kushughulikia miradi mingine ya maji kwenye sehemu ambazo zina uhaba wa maji.

Akiongea  na waandishi wa Habari ofisini kwake mtaa wa Miomboni Mjini Babati, Mkurugenzi Mtendaji wa BAWASA Mhandisi Iddy Msuya alisema kuwa ongezeko hilo la asilimia 36 ni sawa na bei ya  shilingi 1,748 kwa unit moja ya maji, bei ambayo ni ndogo ukilinganisha na mikoa mingine.

"Sisi kama BAWASA lengo letu la kupandisha bei ya maji hatuna nia ya kuwakomoa wananchi wetu hapana hii ni kuweza kupata fedha za kuweza kukarabati miundombinu ya maji ili ile kero ya kukatika kwa maji  ifutike kabisa ili hata mtu akiamka usiku wa manane akifungulia maji yanatoka.

"Bei ya maji katika  mkoa wa Arusha wenye chanzo cha maji ya mtiririko ni Shilingi 1,500 kwa unit moja sawa na asilima 50 ya ongezeko la bei ya maji hivyo Babati bado iko vizuri" Alisema Msuya.

Kwa mujibu wake hali ya upotevu wa maji imepungua na kufikia asilimia 35 kutokana na juhudi ya mamlaka ya BAWASA kuboresha miundo mbinu ya mabomba ya zamani ambayo baadhi yao  iliwekwa katika kipindi cha Uhuru ambayo imechoka na kupoteza maji mengi.

Alisema  kwa utaratibu BAWASA inapotaka kuongeza bei ya maji kwa walaji wake huomba mapendekezo ya ongezeko hilo la maji EWURA ambao  huchukua mapendekezo kutoka kwa wadau na kuyapeleka Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa ajili ya kutoa kibali cha ongezeko hilo.

Mhandisi Msuya alifafanua kuwa BAWASA walipendekeza   kuongeza bei kwa shilingi 2,175 kutokana na gharama za uendeshaji lakini baada ya kukusanya maoni ya Walaji na EWURA bei pendekezwa ilikuwa ni Shilingi 1,748 bei ambayo  haikufanikiwa.

Msuya alibainisha kuwa kupanda kwa bei ya maji huwa inatolewa maelekezo mfano kununua mita za maji zipatazo 5,000, kuongeza mitandao ya maji kutoka Ng'wang'warai kuelekea shue ya msingi Tarangire na kujenga machujio ya maji ya kijiji hicho na Mutuka.

hata hivyo alisema ni azma ya serikali ya kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2020 upatikanaji wa maji ufikie asilimia 100 kwa wananchi waishio vijijini na kwamba BAWASA imejiwekea lengo la kuhakikisha wakazi wake wanapata maji kwa uhakika bila mgao au kulazimika kuchota maji.

Baadhi ya wananchi wa mji wa Babati walisema BAWASA haijawatendea haki kwani hawakushirikishwa kuongezeka kwa bei ya maji huku huduma ikiwa hairidhishi kwani hakuna mabadiliko ya huduma kwa kuwa maji yanayotoka ni machafu.

"Maji yanayotoka na ndio tunayoyatumia kwa kunywa, tunakunywa maji machafu sana wametupandishia bei ya maji lakini huduma ndo imezidi kuwa mbaya zaidi, maji yanatoka machafu na tulishawaambia wakasema watafuatilia lakini hadi leo kimya watatusababishia tuumwe matumbo," Alisema Yusufu Mdoe.