Mbinu muhimu za kuzingatia ili kufanikiwa katika biashara

Biashara nyingi zinazoanzishwa haziwezi kufikisha miaka mitano, na hata zinazofikisha huwa hazina maendeleo mazuri.

Hii ni kutokana na sababu biashara nyingi huanzishwa kiholela, kienyeji, kimazoea, ukosefu wa mipango na mikakati ya biashara. Pia, ukosefu wa utafiti wa masoko na kukosa utaalamu na ujuzi mbalimbali katika biashara.

Katika kuanzisha biashara yako unatakiwa kujifunza mbinu na ujuzi mbalimbali kadri unavyozidi kuifanya ili iweze kufanikiwa. Kuna hatua ambazo ukizifuata biashara yako itafanikiwa.

Fanya utafiti
Ukishakuwa na wazo la biashara unayotaka kufanya, kinachofuata ni kuangalia uhalisia, jiulize je, wazo lako lina uwezekano wa kufanikiwa? Unahitaji kuendeleza wazo lako huku ukiendelea kufanya utafiti wa kina ili kupata uhalisia wa wazo lako kabla hujasonga mbele.

Ili biashara ndogo ifanikiwe lazima ilenge kutatua tatizo, kukidhi mahitaji au itoe kitu ambacho soko linahitaji au kuongeza thamani katika biashara husikKuna njia kadhaa zinazoweza kukusaidia kutambua mahitaji hayo, hasa kufanya utafiti na kujaribu.

Kadri unavyotafiti soko, kuna baadhi ya maswali ambayo lazima huyajibu; kuna uhitaji wa bidhaa/huduma yako?; Nani anahitaji?; Kuna mtu au kampuni zinatoa bidhaa/huduma sawa?; Ushindani ukoje? Na namna gani biashara yako itaingia sokoni?

Tengeneza mpango wa biashara
Ili biashara yako iweze kufanikiwa huna budi kuwa na mpango wa biashara wa namna ya kulifanyia kazi wazo lako. Mpango wa biashara ni muongozo utakaokuongoza katika biashara yako kuanzia hatua ya awali hadi inavyokua.

Mpango wa biashara unaweza kukupa dira sahihi ya kile unachotegemea kufanikiwa katika biashara yako na namna gani umepanga kufanya kitu hicho kiuhalisia, unaweza pia kutengeneza mpango kazi katika daftari lako na ukaendelea kuboresha kadri mda unavyosonga mbele.

Pangilia matumizi fedha
Kuanzisha biashara ndogo hakuhitaji fedha nyingi sana, lakini itakuhitaji kufanya baadhi ya uwekezaji muhimu wa mwanzo kama vile ufahamu wa biashara husika na uwezo wa kugharimia kadri unavyoendelea kabla hujaanza kupata faida.

Weka pamoja daftari linaloonyesha makadirio ya gharama ya kuanzisha na kuendeleza biashara yako kama vile vibali, leseni, ada, ushuru, bima, vifaa, utafiti wa soko, matangazo, mshahara wa wewe binafsi na wasaidizi wako, gharama ya pango, uzalishaji, gharama za usafirishaji na usambazaji.

Chagua mfumo wako wa uhasibu
Biashara ndogo zinaendeshwa vyema na kwa mafanikio zaidi ikiwa kuna mifumo rasmi ya kifedha, mapato na matumizi ikifanya kazi kwa weledi na kibunifu. Moja ya mifumo muhimu zaidi katika biashara ndogo ni pamoja na mfumo imara wa uhasibu.

Mfumo wako wa uhasibu ni muhimu ili kuunda na kuongoza bajeti yako, kupanga viwango na bei, kufanya biashara na wengine pamoja na kodi.

Tengeneza eneo la biashara
Kuandaa eneo lako la biashara ni muhimu sana katika uendeshaji wa biashara yako iwe ni kwenye ofisi yako nyumbani, ofisi binafsi ya biashara au eneo lolote biashara yako inafanyika.

Inakubidi ufikirie kwa kina kuhusu eneo, vitendea kazi na mengineyo yote yanayohusika katika biashara yako, hakikisha eneo la biashara yako linafaa kwa aina ya biashara utakayokuwa unafanya.

Andaa timu yako
Ikiwa utakuwa unaajiri watu mbalimbali wa kukusaidia katika biashara yako, basi ni wajibu wako sasa kuanza kutengeneza timu yako.

Hakikisha unapata muda wa kutosha kuainisha nafasi, wajibu na sifa unazozihitaji katika kila kitengo cha biashara yako. Utawala wa biashara ndogo una muongozo rahisi katika kuajiri watu kitu ambacho ni muhimu kwa mwenye biashara ndogo kukua na kufanikiwa.

Tangaza biashara yako
Ikiwa biashara yako tayari imeanza huna budi kuanza kuvuta wateja katika huduma/bidhaa yako. Utahitajika kuanza na mbinu na mikakati ya kimasoko na mauzo ya kipekee sana ili kuweza kufikia wateja.