Mfumko wa bei wapanda Mei

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imetoa taarifa ya mfumuko wa bei ya bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi nchini ambao umepanda hadi kufikia asilimia 3.5 kwa mwaka ulioishia mwezi Mei kutoka 3.2 ya mwaka ulioshia mwezi Aprili.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, mkurugenzi wa shughuli za kitakwimu kutoka NBS, Irenius Ruyobya alisema ongezeko hilo la mfumuko wa bei limetokana na kupanda kwa bidhaa za chakula na zisizokuwa za chakula.

Alisema hiyo inamaanisha kuwa kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Mei 2019 imeongezeka ikilinganishwa na kasi iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili 2019.

“Baadhi ya bidhaa za chakula zilizochangia kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa mwezi Mei ni pamoja na unga wa mahindi  kwa asilimia 2.8, nyama kwa asilimia 4.7, samaki kwa asilimia13.5,  matunda kwa asilimia 15.3, viazi mviringo kwa asilimia 21.7 na mihogo mibichi kwa asilimia 24.8,” alisema Ruyobya.

Alizitaja baadhi ya bidhaa zisizokuwa za chakula ambazo zimesababisha mfumuko wa bei kwa mwaka unaoishia mwezi Mei mwaka huu kuwa ni mavazi na viatu kwa asilimia 3.7, mkaa (13.1), vyombo vya jikoni (2.5), gharama za kumwona daktari kwa hospitali binafsi  (6.4), dizeli (11.1) na petroli kwa asilimia 4.2.

Alisema mfumuko wa bei kwa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Mei mwaka huu umeongezeka hadi asilimia 2.2 kutoka asilimia 0.9 kwa mwaka ulioishia mwezi Aprili mwaka huu.