Loading...

6/14/2019

Mtoto akutana na familia yake baada ya miaka 40

Mwanamume ambaye wazazi wake walitekwa na majasusi mnamo 1977 amekutana na familia yake kwa mara ya kwanza baada ya miaka 40.

Javier Darroux Mijalchuk alikuwa na miezi minne wakati babake na mamake aliyekuwa mja mzito walipotoweka huko Buenos Aires.

Baadaye aliasiliwa na familia ambayo haikujua kuhusu wazazi wake.

Lakini miaka michache iliyopita, alianza kuingiwa na shaka kuhusu utambulisho wake asili, na akaomba usaidizi kutoka shirika la haki za binaadamu 'Grandmothers of the Plaza de Mayo'.

Kundi hilo huwatafuta watoto wa vizazi vya watu waliouawa au kutoweshwa kwa lazima wakati wa utawala wa kidikteta wa kijeshi, uliodumu tangu 1976 hadi 1983, na huwakutanisha na wazazi wao.

Darroux ni mtoto wa 130 ambaye shirika hilo lilifanikiwa kumtambua baada ya kufanya vipimo vya DNA.

Akizungumza na waandishi habari, alimshukuru mjombake Roberto Mijalchuk, ambaye anasema alikuwa akimtafuta kwa miaka arobaini iliyopita.

"Kujulikana upya kwa utambulisho wangu ni heshima kwa wazazi wangu, jambo linaloniliwaza, ni ishara ya kumbukumbu, ukweli na haki," amesema Darroux.

"Ni kiashiria kwamba, kama inabidi nieleze kwa kutumia wakati, hakuna muda muhimu maishani mwangu kama nilipomkumbatia mjombangu, ambapo baada ya kunitafuta kwa miaka 40 alichoweza kuniambia ni: 'Wewe ni Javi?' na alinikumbatia kama vile ambavyo hakuna mtu amewahi na hakuna atakayewahi kunikumbatia kwa namna hiyo."

Ameongeza kwamba sasa atajaribu kutafuta taarifa zaidi kuhusu wazazi wake, Juan Manuel Darroux na Elena Mijalchuk.

Takriban watu 30,000 waliuawa na jeshi la junta nchini Argentina.
Loading...