Saudi Arabia yaikataa ripoti ya Umoja wa Mataifa kuhusu mauaji ya Khashoggi

Saudi Arabia imeikataa ripoti iliyotolewa na Umoja wa Mataifa ikisema kuna ushahidi wa kutosha kwamba Mwana Mfalme Mohammed bin Salman, pamoja na maafisa wengine wa ngazi ya juu walihusika katika mauaji ya mwandishi wa habari Jamal Khashoggi.

Hakuna chochote kipya, alisema waziri wa mambo ya nje wa Saudi Arabia Adel al-Jubeir kupitia ukurasa wake wa twitter na kuongeza kuwa ripoti hiyo iliyochapishwa na kusambazwa katika vyombo vya habari ni ya kutatanisha na imejaa madai yasiyo na msingi.

Mtaalamu maalum wa kisheria wa Umoja wa Mataifa anayechunguza mauaji Agnes Callamard, amefikia maamuzi kwamba mauaji ya mwandishi huyo yalikuwa ya makusudi na yaliyopangwa.

 Ripoti yake imeegemea katika sauti zilizorekodiwa na kazi ya kitaalamu iliyofanywa na wachunguzi wa Kituruki sambamba na taarifa za washukiwa nchini Saudi Arabia.