Aliyetoka CHADEMA kwenda CCM alalamika kuambiwa hatorudi 2020


Mbunge wa Simanjiro kupitia CCM James Ole Milya, ambaye alihamia chama hicho akitokea CHADEMA, ameeleza kutishiwa na baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Manyara, kuwa hawezi kurudi tena kugombea jimbo hilo, kwa kile alichokidai watu hao wana ukaribu na baadhi ya viongozi wa juu.

Mbunge Ole Milya ametoa kauli hiyo mkoani Manyara, wakati wa mkutano wa hadhara ambao ulihudhuriwa na Waziri wa Madini Dotto  Biteko, ambapo Mbunge huyo alitoa madai mbalimbali akimtuhumu Mkuu wa Mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti.

"Naambiwa kuna ripoti inatoka wiki ijayo ikimshambulia Mbunge, kuwa anatetea baadhi ya watu, nimepiga kelele kama Mbunge muda mrefu sitaki wananchi wangu waendelee kuteswa, kwa sababu ya watu wachache wanaofanya mambo ya hovyo" amesema Mnyeti.

"Sisi wengine ambao tunatafuta kura eti kwa sababu kuna viongozi hapa wanaukaribu na kiongozi wa juu wa chama na nchi, sisi 2020 hatutakuwa Wabunge, eti atafanya vituko, tuko tayari kutokuwa Wabunge lakini haki ya watu isimamiwe." amesema Ole Milya.

Akijibu madai hayo Mkuu wa mkoa wa Manyara Alexander Mnyeti, ameeleza kuwa anataarifa kuwa Mbunge huyo amekuwa akitumia silaha za moto, kuomba fedha kwa wachimbaji.

"Nimehangaika sana watu kuajiriwa kwenye eneo hili, kama nimekosea kwa hili sistahili kutukanwa hadharani, kwa sababu hiki kilio kimetoka kwenu, nashangaa sana leo kimegeuka kwangu." amesema Mnyeti.

"Mimi sina njaa, hata wakati naanza utumishi kama Mkuu wa Wilaya sikuwa na njaa, zaidi nina kesi zaidi ya nne, Mbunge anawatolea bastola wachimbaji ili wampe pesa, nitawataja, mkitaka tufike huko niko tayari kufika." amesema Mnyeti.