CHADEMA wampeleka Mwenyekiti wao CCM


Na Omary Mngindo-Bagamoyo

Katika hali isiyo ya kawaida wakazi wa Kitongoji cha Nyakahamba Kata ya Kerege Bagamoyo Mkoa wa Pwani, wamemhamisha Mwenyekiti wao Franck Masiaga, kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Kitongoji cha Nyakahama chenye wakazi zaidi ya 400 ambao katika uchaguzi wa mwisho walimchagua Masiaga kuwa Mwenyekiti wa tiketi ya CHADEMA, wamefikia hatua hiyo baada ya kubaini kutopatiwa ufumbuzi wa changamoto za kimaendeleo zinazowakabiri.

Wakizungumza na waandishi wa habari baada ya Masiaga kukabidhi kadi ya chama hicho kisha kuchukua ya CCM, wakazi Neema Yusufu, Karuma Athumani, Said Ally na Imani Ramadhani walisema kuwa kwa kipindi hicho tangu kumchagua Masiaga hawana huduma ya maji safi, umeme wala barabara.

"U-CHADEMA wetu tumeweka kando, tukamshawishi Mwenyekiti wetu arejee CCM ili tuondokane na adha zinazotukabili, kwetu hakuna maji, umeme na barabara yenyewe haina kiwango, tumemshauri nae ametukubalia," alisema Neema.

Katika hafla hiyo chini ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Bagamoyo Abdul Sharifu aliyempokea Masiaga na wana- Nyakahamba 300, Sharifu alisema kwamba hatua ya wanasiasa hao kujiunga na chama hicho inaonesha kukubalika kwa utendaji wa Mwenyekiti wa Taifa Dkt. John Magufuli.

"Niwapongeze kwa uamuzi wenu wa busara wa kujiunga na chama ambacho ndio kimbilio la wananchi wanyonge, nadhani mmaona kazi kubwa inayofanywa na chama chetu chini ya Rais John Magufuli, karibuni tukijenge chama na nchi yetu," alisema Sharifu.

Masiaga mbele ya viongozi mbalimbali akiwemo diwani wa Kata hiyo Said Ngatipula, alisema kuwa tangu achaguliwe kushika wadhifa huo miaka minne iliyopita hakupata ushirikiano kutoka kwa viongozi wa chama hicho, hali iliyomweka kwenywe wakati mgumu wa kutekeeleza majukumu yake.