Hatimaye mshambuliaji wa zamani wa Liverpool ampata mbwa wake aliyepotea

Mshambuliaji wa zamani wa Liverpool Daniel Sturridge amesema ana furaha isiyo kifani kwa kumpata mbwa wake aliyepotea aitwaye Lucci.

Sturridge, 29, alisema yupo tayari kutoa kiwango chochote cha pesa ili kumpata mbwa huyo ambaye alipotea baada ya nyumba yake nchini Marekani kuvunjwa na wezi.

Video na picha za mbwa huyo zilichapishwa mitandaoni na baada ya hapo akarejeshwa kwa mmiliki wake halali.

"Siamini," Sturridge amesema katika video aliyochapisha kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram.

"Nataka tu kusema asante kwa kila mtu mitandaoni aliyeniunga mkono na kupaza sauti. Ninashukuru sana."

Sturridge hata hivyo ahakusema kama alitoa pesa kwa mtu aliyemrejesha.

Awali mchezaji huyo alisema tukio hilo limetokea alipokuwa kwenye matembezi Jumatatu usiku.

"Tutalipa kiasi chochote kile ili kumpata mbwa wetu," amesema Sturridge.

"Yoyote atakayemrudisha mbwa wangu (atapata) elfu 20, elfu 30 (pauni), kiasi chochote kile."

Sturridge pia ametuma picha nne za mbwa huyo na pia video zinazoonesha wanaaume watatu waliojifunika uso wakiingia kwenye nyumba hiyo.

Sturridge, kwa saasa anahusishwa na uhamisho kuelekea klabu ya Aston Villa ambayo inarejea EPL msimu ujao utaoanza Agosti.