Jeshi la Iran lakana kuizuwia meli ya mafuta ya Uingereza

Mkuu wa majeshi ya Ufaransa Francois Lecointre amesema leo baada ya Uingereza kuishutumu Iran kuzisumbua meli za mafuta za nchi hiyo kuwa, hali ya wasi wasi katika eneo la Ghuba haielekei kufikia kiwango cha kutoweza kudhibitiwa.

Lecointre amesema hata hivyo kuna hali ya kupimana nguvu kati ya Marekani na Iran, ambayo inaweza wakati wowote kufikia hatua ya kutoweza kudhibitika.

Serikali ya Uingereza imesema leo kuwa meli tatu za Iran zilijaribu kuzuwia njia ya meli ya mafuta ya Uingereza katika eneo la maji la Ghuba, na kulazimisha meli ya kijeshi ya Uingereza HMS Montrose kuingilia kati.

Jeshi la Iran lilikana kuwa limeizuwia meli ya mafuta ya Uingereza katika mlango bahari wa Hormuz.

Jeshi la kimapinduzi ya Iran limesema katika taarifa kuwa hakukuwa na makabiliano katika muda wa masaa 24 na meli yoyote ya kigeni, ikiwa ni pamoja na meli za Uingereza.