Mahakama yapendekeza makosa yote kuwa na dhamana


Mahakama ya Tanzania inapendekeza makosa yote kuwa na dhamana kwa kuwa hatua hii itasaidia kuondoa msongamano wa Mahabusu kwenye Magereza mbalimbali nchini.

Akizungumza na Waandishi wa habari mara baada ya kuwakubali na kuwaapisha wanasheria waliomaliza mafunzo ya Sheria kwa vitendo kuwa Mawakili, jijini Dar es salaam leo, Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma ameyataja baadhi ya mapendekezo ya Mahakama yatakayosaidia kuondoa msongamano magerezani kuwa ni pamoja na upelelezi wa kesi kumalizika mapema.

Jaji Mkuu alisema Mahakama imekuwa ikilaumiwa kwa kuchelewesha kesi mahakamani lakini kinachosababisha kuchelewa kwa mashauri hayo ni upelelezi kutokukamilika kwa wakati.
“Kuchelewa kumalizika kwa shauri Mahakamani wa kulaumiwa ni wapelelezi na siyo Mahakama”, alisema Jaji Mkuu.

Alisema pendekezo jingine ni sheria kutamka wazi muda wa kufanya upelelezi yaani ikifika muda fulani upelelezi haujakamilika basi shauri hilo lifutwe mahakamani.

Alisema sheria zimeegemea zaidi kwenye adhabu kubwa huku akitolea mfano wa mashauri ya mauaji, matumizi ya dawa za kulevya, Uhujumu uchumi na ubakaji. Aliongeza kuwa mashauri haya yana adhabu kubwa na upelelezi wake huchukua muda mrefu.

Alisema ili kutatua changamoto ya msongamano wa mahabusu magerezani, Mahakama ya Tanzania pia inapendekeza masharti ya dhamana kulegezwa na kushauri kutumiwa kwa vitambulisho vya Taifa kwenye dhamana.

“Hivi sasa wananchi wengi wana vitambulisho vya Taifa ambavyo vinaweza kutumika kama dhamana bila ya kumtaka mwananchi aonyeshe mali”, alisema Prof. Juma.

Jaji Mkuu alitoa mapendekezo hayo ya Mahakama alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na waandishi wa habari waliotaka kufahamu Mamlaka ya kutoa Mahabusu gerezani. Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, Mahakama ndiyo yenye Mamlaka.

Hivi karibuni, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliagiza kufanyika kwa uhakiki ili kubaini mahabusu na wafungwa waliobambikiwa kesi hatimaye kuachiwa huru. Watakaonufaika na matokeo ya uhakiki huo ni mahabusu wenye kesi ndogondogo na wafungwa watoto, wazee, na makundi mengine yenye mahitaji maalum.

Jumla ya wanasheria 720 wamekubaliwa na kuapishwa kuwa Mawakili wakiwemo Majaji nane wa Mahakama ya Rufani, Majaji saba wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Majaji wastaafu watatu, Manaibu Wasajili kadhaa, Mahakimu pamoja na wanasheria wengine.

Hii ni mara ya 60 kwa Mahakama ya Tanzania kuwakubali na kuwaapisha Mawakili wapya. Kwa mara ya kwanza Mahakama ya Tanzania iliwakubali na kuwaapisha Mawakili wapya mwaka 1986.