Loading...

7/11/2019

Majambazi saba wakamatwa Dar


Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar Es Salaam, linawashikilia watu saba kwa tuhuma za wizi wa bajaji maeneo ya Ukonga. Watuhumiwa hao ni Said Salum (27), Amo Kefas (30), Said Ahmad (38), Mohamed Musa (31),Mboke Samwel (26),Abdallah Kipaneli(25) na Mfaume Mussa (25).

Mnamo tarehe 9 Julai 2019 majira ya saa nane usiku huko maeneo ya Kibeberu na Magole  Ukonga watuhumiwa hao walivunja maduka matatu na kufanikiwa kuiba bidhaa mbalimbali, fedha pamoja na bajaji mbili zenye namba za usajili MC 312 CFB aina ya TVS na MC 540 CED aina ya TVS zote zikiwa na rangi ya bluu.

Baada ya wizi huo taarifa zilipokelewa katika kituo cha Polisi Stakishari na upelelezi ulianza maramoja ambapo mnamo tarehe 9 Julai 2019 majira ya saa tano asubuhi watuhumiwa walikamatwa huko maeneo ya Hondogo Gogoni Kiluvya wilaya ya Ubungo.

Aidha watuhumiwa hawa wamekuwa wakifanya matukio ya uhalifu kwa kutumia gari aina ya Toyota Harrier  nyeusi yenye namba T.666 DJG ambayo inashikiliwa na Jeshi la Polisi ili kubaini mmiliki wake.

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa Watuhumiwa wote watafikishwa mahakamani hivi karibuni.

Loading...